Jacquiline Mrisho, MAELEZO
Gaudencia Simwanza |
MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imewashauri
wazalishaji wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba kujiunga katika
vikundi ili waweze kupata mafunzo kwa urahisi pamoja na kusaidiana kiuchumi.
Wito huo umetolewa jana Dar es Salaam na
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa Mamlaka hiyo, Gaudencia Simwanza, alipokuwa
akitoa semina kwa kinamama wajasiriamali iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo
ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Gaudencia alisema ni lazima kuchunguza
kwa makini bidhaa mbalimbali zinazohusisha afya ya binadamu kwa ajili ya kudhibiti ubora, usalama na
ufanisi wa bidhaa hizo ili zisiweze kumdhuru mtumiaji hivyo, mamlaka hiyo
haijawekwa kwa bahati mbaya bali ina madhumuni thabiti ya kulinda afya ya
watumiaji wa bidhaa hizo.
“Ili kuhakikisha bidhaa hizo ni salama
kwa afya ya mtumiaji ni lazima kuhakikisha tunatoa elimu na mafunzo kwa
wazalishaji ili waweze kuzalisha
kulingana na utaratibu mzuri uliowekwa ndio maana tunawashauri wajiunge kwenye
vikundi ili iwe rahisi kupata elimu pamoja na kupata nafasi kubadilishana
mawazo yanayohusu uzalishaji wa bidhaa zao,” alisema Gaudencia.
Aliongeza kwamba kwa sifa ya kwanza ya
kusajiliwa na Mamlaka hiyo ni kuwa na jingo la uhakika na salama kwa ajili ya
kuzalishia bidhaa hizo, hivyo uundaji wa vikundi vya pamoja utasaidia
wazalishaji kutafuta fedha kwa pamoja kwa ajili ya kupata jengo kwani
wazalishaji wengi wamekua wakilalamika kukosa fedha kwa ajili ya jengo la
kufanyia shughuli hizo.
Alifafanua kuwa mbali na vikundi hivyo, TFDA
imekua ikitoa elimu kwa wajasiliamali mbalimbali kupitia ofisi za za kanda zilizopo
katika mikoa saba nchini akizitaja kuwa ni Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za
Juu Kusini, Kanda ya Mashariki, Magharibi, Kaskazini, Kusini na Kanda ya Kati.
Aliwasisitiza wajasiriamali wote
wanaozalisha bidhaa zinazohusisha afya ya binadamu kusajili majengo yao pamoja
na kusajili bidhaa zao ili kupata Hati ya Usajili wa Jengo pamoja na kibali cha
kutengenezea bidhaa hizo mara baada ya kukamilisha taratibu zote zilizoainishwa
kisheria.
TFDA ni taasisi iliyopo chini ya Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyoundwa kwa ajili ya
kusimamia na kuhakikisha bidhaa zinazohusika na afya ya mtumiaji zinatengenezwa
katika hali ya usafi na usalama.
0 comments:
Post a Comment