Jemah Makamba
MSHITAKIWA Emmanuel Mkenya aliyefikishwa kwenye Mahakama
ya Mwanzo Kariakoo jana kusomewa mashitaka ya uzembe na uzururaji, ametoroka
mikononi mwa polisi baada ya kujipaka kinyesi mwilini.
Mshitakiwa huyo alifikishwa asubuhi mahakamni hapo kujibu
mashitaka yanayomkabili na kuwekwa mahabusu kusubiri kuitwa.
Muda wa kusomewa kesi ulipofika, askari alikwenda kumwita
yeye na wenzake ili wapande kizimbani, lakini mshitakiwa huyo alitoka akiwa
amejipaka kinyesi chake, alichojisaidia kwenye choo cha ndani ya mahabusu.
Huku akionekana kujiamini, mshitakiwa huyo badala ya
kupanda kizimbani, aliondoka taratibu kupitia lango la kutoka nje ya Mahakama,
huku polisi wakishindwa kumkamata kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Baada ya kutoka nje, mshitakiwa mwenzake kwenye kesi hiyo
ya uzembe na uzururaji, alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Agnes Barasobian.
Hata hivyo, kabla ya Karani Hatanawe Kitogo kusoma
mashitaka dhidi ya mshitakiwa wa pili, Hakimu Agnes aliuliza alikokuwa mshitakiwa
namba moja.
Polisi aliyekuwa mahakamani hapo alimjibu Hakimu kuwa mshitakiwa
huyo alitoroka baada ya kujipaka kinyesi mwili mzima.
Hakimu Agnes akionesha kukasirika, alimtaka askari huyo ahahakishe
mshitakiwa anatafutwa na kukamatwa, kwani haiwezekani aondoke mahakamani huku
akiwa na mashitaka yanayomkabili.
Alisema hakubaliani na sababu za askari huyo, kwa kuwa
anatambua kuwa kwenye mafunzo ya kijeshi, hupewa mbinu za kukabiliana na
washitakiwa.
Washitakiwa hao walikamatwa na Koplo Luseseko Januari 19
Msimbazi, Dar es Salaam wakituhumiwa kwa uzururaji. Kesi hiyo iliahirishwa jana
hadi Januari 30 itakapotajwa.
0 comments:
Post a Comment