*Magufuli ataka wanaopenda kuona gwaride kulifuata huko
*Afuta
dhifa ya Ikulu kwa lengo lile lile la kubana matumizi
Waandishi Wetu
Rais John Magufuli |
RAIS Dk John Magufuli amesema kuanzia
mwakani maadhimisho ya sherehe za Uhuru yatafanyika Dodoma.
Aidha, ameweka bayana kuwa sherehe za
mwaka huu zilitumia gharama ndogo, ikilinganishwa na za miaka iliyopita.
Rais Magufuli alisema hayo jana wakati
wa maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, yakiwa
na kaulimbiu ya:
‘Tuunge mkono jitihada za kupinga rushwa
na ufisadi na tuimarishe uchumi wa viwanda kwa maendeleo yetu’.
Alisema sherehe hizo zitakuwa za mwisho
kwa wakazi wa Dar es Salaam kuzishuhudia kwenye uwanja huo na atakayependa kuona
gwaride atapaswa kwenda Dodoma.
“Hizi ni sherehe za mwisho hapa Dar es
Salaam, hivyo atakayekuwa anataka kushuhudia gwaride ajiandae kwenda Dodoma,”
alisema.
Alisema sherehe za miaka 55 zilitumia
gharama ndogo na hakukuandaliwa chakula, hivyo baada ya sherehe za uwanjani
kila mtu alirejea nyumbani.
“Tukimaliza hapa tumemalizana, hakuna
chakula kama zamani, lakini tumeamua kuifanyia hapa, kwa sababu itakuwa ya
mwisho hapa, mwakani itafanyika Dodoma,” alilisitiza.
Rais alisema sherehe za Uhuru ni muhimu na
miaka 55 imeshuhudia mafanikio mengi, ikiwamo kulinda mipaka, kudumisha amani,
umoja na mshikamano kwa wananchi.
Alisema Watanzania wamekuwa wakiishi
bila kubaguana kidini, kirangi, kikabila wala itikadi za vyama, jambo ambalo
linapaswa kudumishwa na kila Mtanzania.
Aidha, alisema katika kipindi cha miaka
55 walijenga miundombinu ya barabara,
madaraja, meli, viwanja vya ndege, maji na huduma za kijamii.
Rais Magufuli alisema watangulizi wake
walifanya mambo mengi ambayo yataendelea kupongezwa na kuenziwa na vizazi
vijavyo.
Alisema pamoja na mafanikio hayo, bado
zipo changamoto ambazo walikutana nazo, hivyo na atajitahidi kukabiliana nazo
kwa kipindi chake.
Rais alisema bado rushwa na umasikini ni
mambo ambayo yanasumbua jamii, hivyo yeye na wasaidizi wake, wamedhamiria
kufanya kazi kwa nguvu zote ili kuwakomboa na kusisitiza kuwa kila mwananchi
anapaswa kufanya kazi katika eneo lake.
Halikadhalika alisema wazee 17 ambao
walijitolea kupigania Uhuru wakiongozwa na marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere walionesha ujasiri na uzalendo, hivyo na vizazi ambavyo
havijashuhudia kupatikana kwa Uhuru vinapaswa kujifunza.
Kuhusu mwaka jana kutofanyika sherehe,
alisema gharama zilikuwa kubwa hali ambayo ilimpa wasiwasi na kuelekeza fedha
za shughuli hizo zitumike kupanua barabara ya Ali Hassan Mwinyi hadi Mwenge.
Alisema kutokana na uamuzi huo aliagiza
watu kufanya usafi wa mazingira siku hiyo jambo ambalo liligusa jamii nzima.
“Sh bilioni 4 kutumika kwenye sherehe na
posho ya siku moja ni nyingi sana, halafu fedha zenyewe zinatumika kwa watu
wachache, ndiyo maana nikazielekeza kwenye barabara, ili ziguse Watanzania wengi,
nadhani hata nyie mnaona,” alisema.
Aidha, alisema wakati wa sherehe hiyo,
alikuwa hajakamilisha kuunda Serikali yake jambo ambalo kwa sasa halipo na
hawezi kuacha kuadhimisha siku hiyo kutokana na umuhimu wake.
Kwa upande mwingine, alisema wakati wa
kampeni waliahidi kwenye Ilani ya CCM,
mambo mengi ambayo wananchi waliyakubali na kuwapa kura, hivyo ni wakati wa
kutekeleza kwa nguvu zote.
“Tuliahidi viwanda, kupambana na rushwa,
ufisadi na kutanua huduma za jamii hasa maji, hivyo kupitia bajeti ya maendeleo
ambayo ni asilimia 40 ya bajeti ya Sh trilioni 29.5 tumeanza kutekeleza,”
alisema.
Alisema tayari zabuni ya kujenga reli ya
kisasa imetangazwa na utaanza na kilometa 200 ili kuunganisha na nchi jirani za
Rwanda na Burundi.
Halikadhalika upande wa anga alisema
wamenunua ndege sita; tatu ni Bombardier Q 400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76,
zingine zina uwezo wa kubeba abiria 137 hadi 150 na Boeing moja ya abiria 250.
“Tumefanya hivyo kwa lengo la kuongeza
uchumi na utalii wa nchi yetu, hiyo ni baadhi ya mikakati ambayo tunaendelea
nayo kuiletea Tanzania maendeleo,” alisema.
Alisema kwenye afya, Bajeti imeongezeka
kutoka Sh bilioni 31 hadi Sh bilioni 250 huku sekta ya elimu kila mwezi zaidi ya
Sh bilioni 18 zinatumika kutoa elimu bure ya msingi hadi sekondari huku vyuo
vikuu vikipata zaidi ya Sh bilioni 483 kwa mwaka huu, kutoka Sh bilioni 300.
Rais alisema kutokana na utaratibu huo
wa elimu bure, wanafunzi wa shule za msingi waliongezeka kwa asilimia 84 na
sekondari asilimia 26.
Alisema pia kuna ongezeko la makusanyo
ya fedha tangu aingie madarakani ambapo alikuta makusanyo yakiwa Sh bilioni 850
hadi Sh trilioni 1.2.
Changamoto
Aidha, Rais alisema katika mwaka mmoja
amekutana na changamoto za rushwa, ufisadi, watumishi hewa zaidi ya 19,000,
wanafunzi hewa zaidi ya 65,000 na kaya masikini hewa zaidi ya 55,000.
Alilishukuru Bunge na vyombo vya utoaji
haki kwa kupitisha sheria ya kupambana na rushwa na kuahidi kuitumia vema, ili
kuhakikisha anarekebisha mfumo wa utumishi.
Pia alisema Serikali imejipanga kuondoa
uonevu, hasa kwa wananchi wanyonge ili kufaidika na Tanzania yao.
“Ombi langu, Watanzania endeleeni
kudumisha amani, kwani ndiyo msingi wa maendeleo bila hivyo hakuna maendeleo,”
alisema.
Katika maadhimisho hayo, Rais
alisalimiana na viongozi mbalimbali na wananchi waliofurika uwanjani hapo.
Baadhi ya viongozi mashuhuri
waliohudhuria ni Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein, Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Wengine ni Rais mstaafu Alhaji Ali
Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Jaji Mkuu Othman
Chande na mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mama Fatma Karume.
Tofauti na ilivyozoeleka sherehe hizo
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, jana asilimia kubwa ya viongozi wastaafu hawakuonekana.
Rais mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe
Anna, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, pengine kutokana na majukumu aliwakilishwa
na mkewe, Salma ambaye alikuwapo, Spika wa Bunge Job Ndugai, Naibu Spika Dk
Tulia Ackson na mawaziri wakuu wote wa zamani hawakuhudhuria.
Pia viongozi wa vyama vya siasa akiwemo
Katibu Mkuu wa CCM, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, James Mbatia wa
NCCR-Mageuzi na wengine wengi hawakuhudhuria.
Walihudhuria mabalozi wa nchi
mbalimbali, waambata wa kijeshi, mawaziri, makatibu wakuu, Jaji Mkuu, Athuman
Chande, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na wakuu wa vikosi vya
ulinzia na usalama.
Imeandikwa na Suleiman
Msuya na Salha Mohamed
0 comments:
Post a Comment