Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu Kassim Mjaliwa amesema Serikali
imetenga Sh bilioni 15 za mafunzo kwa vijana zaidi 2,500 ili kuwajengea uwezo wa
kuwa nguvukazi kwenye viwanda vinavyotarajiwa kujengwa nchini.
Alitoa kauli hiyo juzi kwenye sherehe za utoaji Tuzo
ya Mwajiri Bora wa Mwaka 2016, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Tuzo hizo ziliandaliwa na Chama Cha
Waajiri Tanzania (ATE).
Waziri Mkuu alisema Serikali imejielekeza kutoa
mafunzo kwenye sekta za kipaumbele kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo
kama kilimo biashara, mafuta, gesi, utalii, usafirishaji, ushonaji na bidhaa za
ngozi.
Alisema jitihada zinaendelea kwenye maeneo mengine
ili waajiri wawe na wigo mpana wa kupata wafanyakazi wenye stadi stahiki, kwa
kuwa Serikali inatambua umuhimu wao kuwa nguvukazi yenye ujuzi na umahiri
mkubwa kwa lengo la kuongeza tija.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia tozo zinazotozwa na mamlaka tofauti za
Serikali kwa huduma zinazofanana, kuwa wanazitambua na tayari mchakato wa
kuainisha sheria zote zinazoonekana kukwamisha uwekezaji pamoja na mazingira ya
biashara nchini.
“Lengo letu ni kuendelea kuboresha mazingira ya
ufanyaji biashara nchini ili yaweze kuvutia zaidi na mchakato huu
unashughulikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango.
“Tunaomba mvumilie na mshirikiane nasi kuendelea kuainisha
sheria zinazokwaza biashara, ili tuweze kuzijumuisha kwenye mapitio hayo,”
alisema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alishauri waajiri nchini
waendelee kufanya kazi kwa mujibu wa
sheria ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima mahala pa kazi.
Pia aliwasihi wafanyakazi kuongeza bidii na
uaminifu ili waajiri waweze kupata faida, na kuwaboreshea maslahi yao.
Alisema: “Tunaposema Hapa Kazi Tu, tunamaanisha
kazi kwenye sekta zote za uzalishaji na utoaji huduma bora nchini, iwe sekta ya
binafsi au utumishi wa umma.
“Nawasihi ndugu zangu Watanzania, wekeni nadhiri
kwamba mwaka 2017 mtafanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuongeza tija na
ufanisi mahala pa kazi.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aliomba
waajiri wawasaidie kuweka msukumo kwenye juhudi za kutoa mafunzo kwa ajili ya
uzoefu na kuongeza ujuzi kwa kutoa nafasi kwa wahitimu kupata uzoefu kwenye
maeneo yao ya kazi.
Hata hivyo, Jenista alisema anatambua umuhimu wa
waajiri na wafanyakazi katika utekelezaji wa sera ya maendeleo ya nchi
hasa kwa kuongeza ajira kupitia sekta ya viwanda kwa asilimia 40 mwaka 2020,
mafanikio ya mpango huo yanategemea mchango wa waajiri wa sekta binafsi.
Pia aliwapongeza ATE kwa kutambua umuhimu wa
kuwekeza kwenye rasilimaliwatu hasa kwa kutoa tuzo katika eneo la kuendeleza
vipaji, ambapo aliomba tuzo zijazo waongeze kigezo cha kupata mwajiri
aliyetumia rasilimali zake kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi wake, ambao ndio
chanzo cha kuinua tija na ushindani kibiashara.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk Aggrey Mlimuka
alisema lengo la uaandaji Tuzo ni kutambua wanachama wenye sera nzuri za
usimamizi wa rasilimaliwatu katika taasisi na kampuni mbalimbali wanachama
nchini.
Alisema kuwa Tuzo hizo zinafuata mbinu za kisayansi na kitaalamu ili kuangalia umuhimu wa rasilimaliwatu katika kampuni za kibiashara kubwa na ndogo na za kati ili kuinua ujuzi wa wafanyakazi.
Alisema kuwa Tuzo hizo zinafuata mbinu za kisayansi na kitaalamu ili kuangalia umuhimu wa rasilimaliwatu katika kampuni za kibiashara kubwa na ndogo na za kati ili kuinua ujuzi wa wafanyakazi.
0 comments:
Post a Comment