Salha Mohamed
KIJANA Said Mrisho (34) anayedaiwa kutobolewa
macho na Henjewele Salum 'Scorpion'(34), amekanusha taarifa za mitandaoni
kuhusika na uhalifu.
Mrisho inadaiwa alifanyiwa kitendo hicho
Septemba 6 saa nne usiku maeneo ya Buguruni, Dar es Salaam, kwa kuchomwa visu
na kutobolewa macho na 'Scorpion' mkazi wa Yombo Machimbo.
Akizungumza na JAMBO LEO jana, Mrisho
alisema anasikitika kusikia taarifa za mitandao kuwa kitendo alichofanyiwa
kinahusishwa na kisasi.
Alisema wanaozungumza hayo ni wenye
mtandao na mtuhumiwa, kwani hata baada ya tukio hilo wapo waliokwenda kumtolea
dhamana alipokamatwa na Polisi.
“Katika maisha yangu, sijawahi kuiba
hata kuku, na sikuweza kutokana na mimi mwenyewe kuwa na ofisi mbili nafanya
kazi zangu,” alisema.
Alisema kuliko watu hao kuzungumza hivyo,
ni vema wakafanya uchunguzi ili kubaini ukweli wa jambo hilo, kwani alisema alikuwa
akiishi na watu vizuri, huku akibainisha kuwa hajawahi hata kupigana na mtu.
Mrisho alisema hata aliyemfanyia tukio
hilo alikuwa hamjui anaitwa nani, kwani alipoulizwa Polisi alimfananisha na
mwizi na kumshambulia.
“Huyo Scorpion alikuwa hanijui, kwa maana
alipoulizwa na polisi alisema hanijui
hata jina ila alinifananisha na mwizi, ndipo alipoambiwa naitwa Saidi na ninakoishi,”
alisema.
Alisema hata wakati hana fedha alikuwa
anaona bora kukopa fedha kuliko kuiba, kwani alikuwa na familia inayomtegemea
na watu wengine nyuma yake.
“Hayo ya kwenye mitandao ya kijamii
hayana ukweli wowote, mimi napenda nifanye kazi…cha muhimu hapo ni kuangaliwa
huyo Scorpion ni nani na kuangalia maisha yake na yangu,” alisema.
Alisema wanaozungumza kwenye mitandao ya
kijamii ni kutaka kumharibia na kuwavunja moyo watu wanaotaka kumsaidia huku
wakimkingia kifua mhalifu.
Mrisho alisema: ”Wapo wanaotaka
kuniharibia hasa kuona Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda ananisaidia na amenipa vitu
ambavyo vitanisaidia kwenye maisha yangu.
“Ukweli utabaki pale pale, kuwa mimi ni
binadamu kama sina nitakopa na sijawahi kuomba, nisipigwe visu au bunduki
sababu mimi si mhalifu,” alisema.
Aliongeza kuwa taarifa za mitandao zinamuumiza
huku akibainisha kuwa Mwenyezi Mungu atamwandikia mema yake na mabaya ya
mtuhumiwa.
“Nashangaa kama alinifananisha na mwizi
kwa nini aliponikamata hakunipeleka Polisi? Na kuamua kunichukulia fedha, mkufu
na hata kunitoboa macho sasa nani mwizi hapo?” Alihoji Mrisho.
Alisema aliyemfanyia kitendo hicho
alikuwa na tamaa ya fedha jambo lililosababisha kumchukulia Sh 300,000, mkufu,
kumchoma visu na kumtoboa macho.
Alisema hajawahi kujihusisha na uhalifu
kwani alikuwa kila akitoka kazini alirudi nyumbani na alipendelea kucheza au
kufanya mazoezi ya soka.
“Hao wanaozungumza ni mtandao wake, ana watu
wengi sana…utashangaa siku ya tukio hakuna aliyekuja kunisaidia pale,
inamaanisha anajulikana, lazima tufikirie huyu ni nani na maelezo yake ya awali
alikubali kunifanyia hivyo, lakini mahakamani alikana,” alisema.
Aliongeza kuwa anaamini kama angekufa
siku ya tukio, hakuna ambaye angejua na angeendelea kuua watu wengi zaidi huku
akibainisha kuwa si mtu wa kutetewa.
“Mimi ni binadamu natenda dhambi na kuna
wakati unaona hii ni dhambi lakini si ya kuua au kuiba, tena mbele za watu,” alisema.
Alishauri mamlaka husika, kufuatilia
mtandao wa mtuhumiwa, kwani ni wa hatari unaoweza kuua hata ndugu na jamaa zao na
kuamini kuwa wapo wengi waliopoteza maisha kwa matukio kama hilo.
Aidha, Mrisho alipewa Sh milioni 12,
bajaji mbili na kuahidiwa nyumba, pikipiki ambavyo hadi sasa bado
hajakabidhiwa.
Kutokana na hali hiyo, Mrisho alisema
anafahamu kuwa Makonda ana majukumu mengi na si yeye pekee wa kumsaidia, bali
husaidia jamii nzima ya mkoa huo.
Hivyo, alisema pikipiki alizomwahidi ziko
nyumbani kwake (Makonda) huku akibainisha kukosekana muda wa kumkabidhi
kutokana na majukumu.
“Ila kodi ya nyumba inaisha mwezi huu (Desemba),
nilitaka kufahamu kama naweza kulipa tena au nitapewa nyumba, ili nisijelipia
nikapoteza fedha na sasa hivi siingizi fedha zinatoka tu,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, JAMBO LEO ilimtafuta
Makonda siku tatu mfululizo, lakini haikufanikiwa kumpata.
0 comments:
Post a Comment