Celina Mathew
Dk John Magufuli |
UTAFITI uliofanywa na taasisi ya Twaweza baada ya Rais
John Magufuli kusaini Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, unaonesha kuwa watu
19 kati ya 20 sawa na asilimia 95, wanataka vyombo vya habari viripoti maovu ya
Serikali iliyo madarakani.
Utafiti huo ni kama umejibu wa taasisi ya Afrobarometer uliofanyika kati ya mwaka 2013
na 2014, ambao ulionesha theluthi mbili ya wananchi sawa na asilimia 65 walitaka
vyombo hivyo kuripoti maovu hayo.
Rais Magufuli alisaini Sheria ya Huduma za Habari ya
mwaka 2016, Novemba 16 baada ya kupitishwa na Bunge la 11 katika mkutano wake
wa tano Dodoma, akisisitiza kuwa itasaidia kuboresha sekta ya habari kwa
manufaa ya wana taaluma na Taifa.
Lakini akitangaza matokeo ya utafiti wao juzi Dar es
Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema takwimu hizo ni
matokeo ya utafiti uliofanyika baada ya kusainiwa kwa sheria hiyo.
Alisema takwimu zilizotumika katika utafiti huo zinatoka
katika vyanzo viwili; sauti za wananchi, uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu
za mkononi, vyote kutoka Tanzania Bara.
Katika ufafanuzi wake, Eyakuze alisema mwaka huu
umegubikwa na changamoto dhidi ya haki za kiraia za kupata taarifa na kutoa
maoni yao kwa uhuru, sambamba na matangazo
mbashara ya Bunge kupitia televisheni na redio kusitishwa, jambo ambalo
wananchi wamekuwa wakilidai kila uchwao.
“Wananchi wengi wanatambua uhuru wa kupata taarifa.
Wananchi wanane kati ya 10 sawa na asilimia 79 wanapinga uamuzi wa Serikali wa
kusitisha matangazo ya Bunge ya moja kwa moja,” alisema.
Aliongeza: “Pia wananchi tisa kati ya 10 sawa na asilimia
92 wanasema ni muhimu matangazo ya Bunge yakarushwa mbashara kupitia luninga na
redio. Wananchi tisa kati ya 10 sawa na asilimia 88 wakisema gharama isitumike
kama sababu ya kusitisha matangazo hayo.”
Alifafanua, kwamba wananchi wanane kati ya 10 sawa na
asilimia 80 walisema uhuru wa kupata taarifa ungesaidia kupunguza vitendo vya rushwa,
idadi kama hiyo wanaunga mkono wananchi kupata taarifa za Serikali.
Kuhusu sheria hiyo, alisema Watanzania kadhaa
wamechukuliwa hatua kali chini ya sheria ya uhalifu wa mitandao kwa kosa la
kutoa maoni yao.
“Vilevile mwaka huu ndipo sheria kandamizi ya Huduma za
Habari ilipitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais,” alisema.
Alisema takwimu hizo zinaonesha, kwamba wananchi
wanathamini sana nguzo kuu tatu za demokrasia imara, uhuru wa vyombo vya
habari, uhuru wa maoni na haki ya kupata taarifa.
Aliongeza kuwa wananchi pia wana uelewa mpana juu ya
madhara ya kuminywa kwa haki hizo muhimu kwa raia, wanaelewa umuhimu wa kuwa na
vyombo vya habari visivyokaliwa kooni.
Alisema ni vema maoni ya wananchi yaheshimiwe na kwamba busara,
hekima, uamuzi sahihi usio na upendeleo pamoja na fikra chanya, vitaongoza
utekelezaji wa sheria hiyo ya huduma za vyombo vya habari.
Aliongeza kuwa kutokana na takwimu hizo wanaiomba Serikali
ifanye busara, kwa kutozidisha makali katika utekelezaji wa sheria hiyo, ili
kupunguza uminywaji wa vyombo vya habari.
“Kwa kuwa taarifa za kuikosoa Serikali zitapungua hali
hiyo itasababisha umasikini wa wananchi kutokuwa na uwezo wa kujua Serikali
inafanya nini na rasilimali zao,” alisema Eyakuze.
Eyakuze ambaye aliainisha utafiti wa Afrobarometer, alisema
unaonesha kuwa asilimia 65 wanataka maovu ya Serikali yaoneshwe, asilimia 31
wanasema utoaji wa taarifa hizo utaiathiri nchi.
Pia, alisema wananchi wanane kati ya 10 ambao ni asilimia
75 wanasema vyombo vya habari vinafanya kazi nzuri ya kufichua maovu na rushwa,
huku wananchi wawili kati ya kumi (18%) wakisema havifanyi kazi vizuri.
Kwa upande wa uhuru wa kutangaza habari, asilimia 53
wanasema vyombo vya habari viwe huru kutangaza habari yoyote huku asilimia 44
wakisema Serikali iwe na mamlaka ya kufungia magazeti yanapochapisha habari zinazoikera
Serikali.
Vilevile, asilimia 65 wanasema vyombo vya habari
havijawahi au kama vimewahi ni mara chache sana, kutumia vibaya uhuru wao kwa
kutangaza vitu vya uongo.
Alisema takwimu za sauti za wananchi za hivi karibuni
zinaonesha asilimia 69 walichagua demokrasia kuliko aina nyingine ya Serikali.
Alisema uungwaji huo mkono wa demokrasia pia unadhihirika
kupitia takwimu za Afrobarometer (mwaka 2014) zinaonesha asilimia 79 ya
wananchi wanasema Serikali inayoongoza kidemokrasia ndiyo wanayoipenda huku
asilimia 81 wakisema ni vema wachague viongozi wao kupitia uchaguzi huru.
0 comments:
Post a Comment