Salha Mohamed
Kamanda Salum Hamduni |
KESI za unyanyasaji wa kijinsia na
ukatili dhidi ya watoto na wanawake zimeripotiwa kuongezeka kwa asilimia 42.3
mwaka huu wilayani Ilala.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam Jumatano
na Jeshi la Polisi Mkoa wa wa Ilala ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya siku 16 ya
kupinga ukatili wa kijinsia yanayotarajiwa kufanyika Desemba 5.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala,
Salum Hamduni, alisema ongezeko hilo linatokana na kupata taarifa za siri za
unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa raia wema kama kutelekeza familia, migogoro
ya ndoa ambapo waathirika wakuu ni wanawake na watoto.
Alisema tayari Polisi imetoa rufaa kwa
kesi 70 kati ya Januari na Septemba kwenda Manispaa kwa Mkurugenzi Kitengo cha Ustawi
wa Jamii huku rufaa 52 zikitolewa katika Januari hadi Desemba mwaka jana.
"Makosa ya jinai yanayojitokeza
kila wakati ni ulawiti, ubakaji, vipigo, shambulio la aibu, shambulio la
kudhuru mwili, lugha ya matusi na shambulio la kawaida," alisema.
Alisema katika maadhimisho hayo,
watashirikiana na Shirika la Kimataifa la Wanawake katiak Sheria na Maendeleo
Afrika (WilDAF), kuandaa maandamano ya amani yatakayoanzia Tazara hadi shule ya
msingi Vingunguti.
"Lengo la maadhimisho hayo ni
kuenzi siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo kampeni kabambe ya
kimataifa inayoongozwa na kituo cha kimataifa cha wanawake katika uongozi kilitenga
siku ya kutetea haki za wanawake tangu Novemba 25, 1991," alisema.
Kamanda Hamduni alisema chimbuko la
kupinga ukatili wa kijinsia na mauaji lilianza baada ya tukio la mauaji ya dada
wa Mirabelle yaliyofanyika Dominica katika visiwa vya Karibeani mwaka 1960.
"Siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia zimekuwa zikitumiwa na Polisi
na wadau duniani kama mbinu mahsusi za kutoa mwito kwa jamii kutokomeza ukatili
dhidi ya wanawake kwa kuelimisha jamiii kuhusu ukatili wa kijinsia na kutoa
taarifa kwenye vituo vya Polisi ili kulinda wanawake na watoto dhidi ya ukatili,”
alisema.
Alisema Polisi imekuwa ikitumika kwenye
maadhimisho hayo kama chombo cha kupaza sauti ili wadau watekeleze wajibu wao
katika kupiga vita na ukatili dhidi ya wanawake.
"Mkoa wa Ilala katika kupambana na
ukatili wa kijinsia na watoto umefungua madawati tisa katika vituo vikubwa vya
Polisi na vya kati yanayotoa huduma kwa jamii dhidi ya vitendo vya ukatili na
unyanyasaji katika vituo vya Ilala, Wilaya ya Kati, Kariakoo, Stakishari,
Buguruni, Pangani, Tabata, Selander Bridge na Vingunguti," alisema.
Alisema mgeni rasmi katika maandamano
hayo atakuwa ni Mkuu wa Wilaya, Sophia Mjema huku akiwataka wananchi kujitokeza
siku hiyo muhimu na ya thamani kwao kwani ulinzi na usalama utakuwa wa kutosha.
Aidha, Hamduni aliomba wananchi hasa
wanawake na watoto kuendelea kutoa taarifa za unyanyasaji na udhalilishaji
katika vituo vya Polisi ili kutokomeza ukatili huo.
0 comments:
Post a Comment