Abraham Ntambara
Raisi John Magufuli |
CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC),
kimemuomba Rais John Magufuli kuachia vyama vya siasa vya upinzani kufanya
shughuli za kisiasa kwa kuwa ni takwa la kisheria.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu
Mkuu Taifa wa chama hicho, Doyo Doyo aliyesema hali ya kisiasa nchini si nzuri
na kwamba Serikali kwa kuendelea kuzuia shughuli za kisiasa ni tishio kwa vyama
kama ADC akisema huenda vikafa.
“Hali ya kisiasa sio nzuri sana, kuna hali ya kutopata
uhuru wa kufanya siasa hasa katika upande wa vyama vya upinzani katika nchi
yetu. Kuzuiwa kufanya mikutano ya kisiasa, makongamano na kadhalika, hii inaua
vyama vya siasa,”alisema na kuongeza:
“ADC inamuomba Rais John Magufuli atuachie tufanye
mikutano kwani jambo hili ni takwa la kisheria.”
Akizungumzia usalama nchini alisema hawaridhishwi na
taarifa za mauaji yanayoendelea Kibiti mkoani Pwani akisema yanatia doa Taifa,
ambapo aliiomba Serikali kujipanga upya na kuweka mkakati madhubuti ya
kukabiliana na wahalifu.
Kuhusu migogoro ndani ya vyama vya siasa Doyo alisema ADC
kinashangazwa na mgogoro wa Chama cha Wananchi (CUF) kushindwa kupatiwa
ufumbuzi wa haraka hali inayofanya wanachama wake kuanza kukata tamaa.
Alisema ADC unachukizwa na hali hiyo kwani kuendelea kwa
mgogoro huo kwa muda mrefu ni kunadhoofisha afya ya upinzani katika macho ya Watanzania.
“Nawaomba Maalim Seif Sharif Hamad na Profesa Ibrahim
Lipumba wakae pamoja ili kumaliza tofauti zao,” alisema Doyo.
Aidha, alieleza kushtushwa kwa ADC na matamko mbalimbali
ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuingilia mgogoro
huo wa CUF.
Doyo aliwashauri Chadema kuacha mara moja kuingilia
mgogoro usiowahusu akidai kitendo hicho cha kuingilia mgogoro huo usiowahusu ni
mkakati wa kisiasa wa kujitengenezea hati miliki ya kisiasa nchini, lakini pia
kinaweza kuhatarisha amani.
Hata hivyo, Doyo alisema alimpongeza Rais Magufuli kwa
juhudi zake anazofanya kuzuia rasilimali za nchi hasa kwa kitendo cha
kuwasilisha miswada kwa hati ya dharura bungeni ili kufanyiwa marekebisho ya
sheria.
0 comments:
Post a Comment