Dotto Mwaibale
Dk Philip Mpango |
SERIKALI
imeitaka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) kuweka
hadharani majina ya wahasibu wabadhirifu ili jamii iwajue.
Hayo yalisemwa juzi
na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Philip Mpango, kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa wakati akizindua Kituo cha Taaluma ya Uhasibu cha Bunju na Kongamano
la Uhasibu la mwaka 2016 la siku tatu Dar es Salaam.
"Ni vizuri
mkaanza kuweka hadharani majina ya wahasibu wasio waadilifu ili jamii iweze
kuwajua," alisema Mpango.
Mpango alisema
kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho, kutaisaidia Serikali kuelekeza fedha
zilizokuwa zikitumiwa na Bodi hiyo kukodi kumbi kwa kazi zake na sasa kupelekwa
kufanya kazi zingine za maendeleo.
"Nawaombeni
mkitunze kituo hiki ili kitimize malengo yake ya kuleta manufaa kwa wananchi na
Taifa kwa ujumla," alisema Mpango.
Aliwataka
wahasibu nchini kutumia taaluma yao kuisaidia Serikali hasa katika kipindi hiki
cha nchi kuelekea kwenye uchumi wa viwanda, badala ya kushirikiana na wafanyabishara
wasio waaminifu kuiibia Serikali.
Mkurugenzi Mkuu
wa NBAA, Pius Maneno alisema katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, walikuwa
wakitumia Sh bilioni 1.5 kwa gharama za kumbi hivyo ujenzi wa kituo hicho
utaondoa changamoto hiyo na kitakuwa pia chanzo cha mapato.
Mpango alisema Serikali
itaendelea ‘kutumbua’ watumishi wasio waaminifu bila kumwonea huruma mhusika na
kuwa atakayebainika atapelekwa Mahakama ya Ufisadi.
Mwenyekiti wa
Bodi ya NBAA, Profesa Isaya Jairo alisema kituo hicho kimejengwa kwa mkopo wa Sh
bilioni 15 kutoka Shirika la Hifadhi ya Taifa (NSSF), Mfuko wa GEPF bilioni 10/-
huku wahasibu na wakaguzi wakichangia bilioni 8/-.
Alisema awali
walikadiria ujenzi huo ungekamilika kwa Sh bilioni 14 lakini kutokana na sababu
mbalimbali, kukamilika kwake kulifikia Sh bilioni 33.
Mwenyekiti wa
Bodi wa GEPF, Joyce Shaidi aliishukuru Serikali kwa ushirikiano na mifuko ya
jamii na NBAA , hasa katika suala la kusukuma mbele maendeleo ya nchi na
kuzitaka taasisi zake kwenda kukodi ukumbi wa kituo hicho cha kimataifa, ili
kusaidia kurejesha fedha zilizokopwa kukijenga.
0 comments:
Post a Comment