Sharifa Marira
Mohamed Mchengerwa |
WAKATI Serikali ikijinadi kuwa ya viwanda, watendaji wake
wamekwenda kinyume kwa kuuza eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanda wilayani
Rufiji, Pwani ekari moja Sh 10,000.
Taarifa ya kuuzwa kwa eneo hilo ilitolewa na wananchi wa
kijiji cha Chumbi wilayani humo kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge Mohamed
Mchengerwa kwa lengo la kushukuru kwa kumchagua na kusikiliza kero zao.
Katika Mkutano huo juzi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wa Wilaya, Mussa Mngeresa alieleza kuwa eneo
hilo lililokuwa na ekari zaidi ya 2,400 liliuzwa kwa Sh milioni 24 hivyo kila moja kwa Sh
10,000 bila wananchi kushirikishwa.
"Uuzwaji huu ulifanywa na Mwenyekiti wa Kijiji cha
Chumbi C ambaye pia ni Diwani wa Chumbi, Salum Mtimbuko (CCM) na alipata baraka za Mkuu wa Wilaya, Juma
Njwayo, ambaye wananchi walimweleza suala hilo kabla, lakini hakulifanyia kazi
na kuwataka waache alichokiita ni majungu,’’ alisema.
Alisema viongozi hao waliudhi wananchi kwa kuuza ardhi
kwa mwekezaji ambaye wanamjua na kwamba ukifanyika uchaguzi wakati wowote kabla
masuala hayo hayajatafutiwa ufumbuzi, CCM itapoteza nafasi, hivyo kumwomba
Mbunge kufanya jitihada za kuleta viongozi wa mkoa, Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi.
Akizungumzia suala hilo, Mchengerwa alilaani kitendo cha
viongozi hao kutaka kukwamisha maendeleo ya viwanda jimboni kwani
alishazungumza na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kuhusu
ujenzi wa kiwanda cha sukari katika eneo hilo.
“Jamani huku ni kurudishana nyuma na kutotambua juhudi za
Serikali na tunaowatetea, haiwezekani viongozi wahusike kuuza ardhi ya kiwanda,
wananchi tusikubali, sheria inaruhusu kuongea upya na mwekezaji huyo, ili
atuachie ardhi yetu au aongeze fedha tukatafute eneo lingine, kuuza Sh 10,000
ekari moja ni aibu,’’ alisema.
Akijibu tuhuma hizo Diwani Mtimbuka alisema: “Nyie
mnanionea wivu, wengine nimewasadia sana kuwalisha na familia zenu, au kwa sababu
mnaniona naishi vizuri na wake zangu wawili na nina nyumba na magari? Pumbavu.’’
Majibu ya Diwani yalizua tafrani kwa wananchi kumzomea na
kumtaka Mchengerwa arudi siku nyingine na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist
Ndikilo, ili atatue kero zilizopo, kwani viongozi wanauza maeneo kiholela na
wanaposhitaki kwa Mkuu wa Wilaya, anakuwa upande wa wauzaji.
Mchengerwa aliwaeleza wananchi hao kwamba ameshawasiliana
na Ndikilo na kuahidi kufanya ziara maeneo hayo Desemba 5.
0 comments:
Post a Comment