Sharifa Marira
Mohamed Mchengerwa |
MBUNGE wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM), amesema atawasilisha
bungeni hoja binafsi ya kupendekeza mabaraza ya ardhi yafutwe, kwa sababu
yanafanya kazi kinyume cha sheria.
Mchengerwa alisema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
katika kijiji cha King'ongo, kata ya Muhoro jimboni humo, baada ya wananchi
kulalamikia mabaraza hayo kuwakandamiza kwa kugawa ardhi yao kwa zaidi ya miaka
30.
"Hilo suala la mabaraza ya ardhi linajulikana kuwa
yanaharibu katika maeneo mengi, yanafanya kazi ya Mahakama kutoa haki ya ardhi,
jambo ambalo ni kinyume na Katiba, nadhamiria kupeleka hoja binafsi katika Bunge
lijalo, kupendekeza mabaraza haya kufutwa,” alisema Mchengerwa.
Sambamba na hilo, alisikiliza kero za wananchi ikiwa ni
pamoja na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, ambayo imekuwa kilio kikubwa cha wananchi wa maeneo yote ya
jimbo hilo, ambapo alisema anaijua changamoto hiyo na ameshaanza kuifanyia kazi
kwa Baraza la Madiwani kuagiza mifugo ambayo ipo kinyume cha sheria kuondolewa
ndani ya siku 30.
Hata hivyo, Mbunge huyo aliahidi kuchangia ujenzi wa
zahanati, shule na barabara kwa kutoa mabati na saruji vyenye thamani ya Sh
milioni 16.
"Nimesikia kero zenu za zahanati, shule na kufukia
madimbwi barabarani; naanza na kuchangia mwenyewe saruji, mabati na fedha
taslimu ili tuanze ujenzi, lakini nakuombeni nanyi mniunge mkono tujenge
pamoja," alisema Mchengerwa.
Pia aliambiwa kero ya kukosekana kwa matuta barabarani, hali
inayosababisha vifo vya watu kwa kugongwa na magari na pikipiki hali ambayo
ilimfanya aoneshe mfano kwa kuweka matuta kadhaa kabla ya kuondoka mkutanoni
hapo.
0 comments:
Post a Comment