UPANDE
wa utetezi katika kesi ya Yusuf Yusuf ‘Mpemba’ (34) umeiomba
Mahakama kuzuia kesi hiyo kuripotiwa na vyombo vya habari huku ukidai kuwa mkuu
wa nchi anaingilia mwenendo wake na kutaka aache kufanya hivyo kwa sababu iko
mahakamani.
Hayo
yalidaiwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Thomas Simba wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na Wakili Aloyce Komba wakati kesi hiyo
ilipokuja ili kuendelea kusikilizwa, lakini ilishindikana baada ya upande wa
Jamhuri kujichanganya katika suala upelelezi.
Komba
aliiomba Mahakama itoe tamko la kuzuia kesi hiyo kuripotiwa, kwa sababu vyombo
vya habari vimekuwa vikiripoti kinyume na mwenendo wake kwa hiyo washitakiwa wana
haki kikatiba kulindwa.
Pia
alidai kuwa hata mkuu wa nchi alishatoa toa tamko kuhusu kesi hiyo ilhali
anajua washitakiwa wameshakamatwa na wako mahakamani na kesi inaendelea.
“Mkuu wa
Nchi nimekuwa nikimsikia akisema kuhusu kesi hii wakati tayari washitakiwa wako
mahakamani,” alidai Komba.
Hata
hivyo, Hakimu Simba alisema hawezi kutoa zuio la kesi hiyo kuripotiwa kwa sababu tayari Mahakama
ilishawapa haki ya kusikilizwa, kwa hiyo kama kuna chombo kimekosea wanachotakiwa
ni kifungua kesi ya madai na si kuzuia.
Kutokana
na Wakili Komba kuonekana kutomwelewa vizuri Hakimu na kuendelea kushinikiza
zuio litolewe, ilimlazimu Hakimu kutoa darasa kuhusu haki za washitakiwa na
vyombo vya habari, hatimaye alikubaliana na alichokisema.
Kabla
malumbano hayo hayajatokea, Wakili wa Serikali, Peter Mwita alidai kuwa
upelelezi haujakamilika hali iliyomshitua Wakili wa Mpemba, Nehemia Nkoko kwa
sababu mara ya kwanza kesi hiyo ilipofika mahakamani, waliieleza Mahakama kuwa
upelelezi umekamilika.
Awali,
Wakili wa Serikali, Paul Kadushi alidai kuwa upelelezi umekamilika na hivi sasa
wanaandaa maelezo ya mashahidi na vielelezo kupeleka Mahakama Kuu Kitengo cha
Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Ufisadi.
Hakimu
Simba alitoa agizo kwa upande wa Jamhuri waweke mipango yao vizuri, na Desemba
15 waieleze Mahakama upelelezi ulikofika na si kutoa taarifa za mgongano.
Mbali na
Mpemba ambaye ni mkazi wa Tegeta washitakiwa wengine ni Charles Mrutu (37) wa
Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa (40) wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima (30)
wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) na Pius Kulagwa (46).
Washitakiwa
hao wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa ujangili na biashara ya meno ya tembo
yenye thamani ya Sh milioni 785.6.
Ilidaiwa
kuwa katika tarehe zisizofahamika kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016 wakiwa
maeneo tofauti ya Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na
mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali vipande 50 vya
meno ya tembo vyenye thamani ya dola za Marekani 180,000 sawa na Sh milioni
392.8 mali ya Serikali bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aliendelea
kudai kuwa katika mashitaka ya pili, Oktoba 26 mwaka huu, washitakiwa wakiwa
Mbagala Zakhem, Temeke, walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye uzito
wa kilo 13.85 na thamani ya dola 30,000 (Sh milioni 65.4).
Ilidaiwa
katika mashitaka ya tatu, kuwa Oktoba 27, wakiwa Tabata Kisukuru walikutwa na
vipande vinne vya meno hayo vyenye uzito
wa kilo 11.1 na thamani ya dola 15,000 (Sh milioni 32.7), huku Oktoba 29 wakikutwa
na viapande 36 vyenye thamani ya Sh milioni 294.6 bila kibali cha Mkurugenzi wa
Wanyamapori.
0 comments:
Post a Comment