Charles James
Tundu Lissu |
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimesema licha ya Rais John Magufuli kupiga marufuku mikutano ya
vyama vya siasa hadi mwaka 2020 kitaendelea kufanya siasa kwa kubuni njia zingine
za kukutana na wananchi tofauti na mikutano ya hadhara.
Hayo yamesemwa na Mwanasheria Mkuu wa Chama
hicho, Tundu Lissu, alipozunguza na viongozi 16 wa vyama vya siasa kutoka nchi
mbalimbali za Afrika ambao wako nchini kwa ziara ya mafunzo ya kisiasa ambayo
yanahusisha pia Chadema.
Lissu alisema ingawa Rais na Polisi
wamepiga marufuku maandamano na shughuli za siasa za hadharani bado wao
wataendelea kupigana kuhakikisha kuwa haki inapatikana bila kujali kama
wanavunja sheria.
“Sisi ni wanasiasa na hiyo ndio kazi
yetu, sasa kama Rais amepiga marufuku tufanyeje? Hatuwezi kwenda kanisani eti
tukasali ili turuhusiwe kufanya mikutano ya hadhara, tunachofanya ni kubuni
mbinu zingine za kukabiliana na watawala na si kujifungia ndani na kukaa
kimya,” alisema Lissu.
Alisema njia ambazo Chadema imepanga
kufanya kuhakikisha kuwa inaendelea kufikia wanachama na wananchi, ni vikao vya
ndani ambapo walianza juma lililopita kwa kanda za Kati na Kusini huku akisema
ni endelevu nchi nzima.
Lissu alisema chama chochote cha siasa
kinapaswa kujifunza kuishi katika mazingira ya kila aina, hivyo ili kuhakikisha
Chadema inaendelea kuwa hai ni lazima ibuni njia mbalimbali za kufanya siasa.
“Vyama vya siasa havipaswi kukaa kimya,
inabidi tufuate mfano wa chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC ambacho
kilizuiwa kufanya siasa mwaka 1960 lakini kikahimili na hatimaye kutwaa
madaraka mwaka 1994, hivyo hata sisi tutahakikisha tunajifungia ndani lakini
kimkakati zaidi,” alisema Lissu.
Mkufunzi wa Mafunzo hayo, Christian
Echle aliishukuru Chadema kwa kuwapa ushirikiano kwa wiki moja waliokuwa nchini,
huku akisema walijifunza vitu vingi kupitia chama hicho.
Mafunzo hayo yalihusisha wanachama na
viongozi 16 kutoka Malawi, Angola, Uganda, Afrika Kusini, Senegal, Ghana,
Namibia, Msumbiji na watatu kutoka Chadema.
0 comments:
Post a Comment