Mary Mtuka, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema
kufika kwa marubani 22 ambao wako kwenye msafara wa ndege za zamani
zilizotengenezwa mwaka 1920 na 1930 utakuwa chachu ya kutangazwa kwa utalii wa
visiwa hivyo.
Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi wa
Masoko na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk Miraji Ukuti Ussi, wakati wa mapokezi
ya msafara wa ndege hizo ambazo ziliwasili visiwani hapa mchana zikitokea
Arusha.
Alisema Zanzibar inajisikia fahari
kupokea marubani wa ndege hizo na kueleza wazi kuwa wanaamini itakuwa chachu ya
utalii wa Zanzibar kwani wengi wanaufuatilia msafara huo.
"Msafara wa ndege hizo unafahamika
kwa jina la Vintage Air Rally na Wazanzibari wengi wamepata nafasi ya kujifunza
kwa vitendo kwa kuona namna ambavyo ndege zilivyokuwa miaka ya zamani.
"Pia ujio wa ndege hizo unafungua
fursa ya kutangaza utalii wetu. Kote ambako msafara huo umepita nchi mbalimbali
duniani zimekuwa zikipata taarifa kupitia vyombo vya habari.
"Na hivyo marubani hao nao watakuwa
sehemu ya kuueleza uzuri wa Zanzibar watakaporudi kwenye nchi zao," alisema.
Ussi alisema Zanzibar inatamani kuona
inakuwa mwenyeji wa kuandaa msafara wa ndege hizo, kwani uwezo huo wanao na
wanaamini hiyo itakuwa nafasi nyingine ya kuileza dunia kuwa uzuri wa Tanzania
na maeneo yake ya utalii.
Pia alisema kitendo cha ujio wa ndege
hizo kisiwani hapa kitachangia ongezeko la watalii visiwani na Tanzania kwa
jumla kutokana na marubani wake kwenda kutembelea sehemu za utalii.
"Tunaamini kuja kwao nchini watakuwa mabalozi wazuri
wanaporejea nyumbani kwao watakwenda kuitangaza Zanzibar kwa kile
watakachokiona, kwani tuna kila sababu ya kwamba mgeni afurahie kuanzia huduma
na anachohitaji," alisema.
Aliongeza kuwa ndege hizo kutua Zanzibar
ni kuutangaza utalii kwani msafara huo unafuatiliwa na mataifa duniani na hivyo
utalii wa Zanzibar nao utafahamika zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Puma
Energy Tanzania Ltd, Philippe Corsaletti
alisema ujio wa ndege hizo ni nafasi nyingine ya kuutangaza utalii wa Zanzibar
na Tanzania kwa ujumla.
"Msafara huo ambao ratiba yake inaonesha
unapita kwenye nchi 10 ikiwamo Tanzania, umefungua milango ya utalii, kwani
marubani watakuwa mabalozi wazuri wa kutangaza utalii
wetu," alisema.
Alisema msafara huo unatamgaza utalii wa
Tanzania kwa kupita kwenye vivutio nchini na kabla ya kuwasili Zanzibar
marubani hao walipita Ngorongoro, Serengeti na kujionea Mlima Kilimanjaro.
"Kabla ya kuondoka Arusha ndege
hizo zilijazwa mafuta aina ya Avigas yaliyotolewa na wadhamini, Puma," alisema.
0 comments:
Post a Comment