Grace Gurisha
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imedai
mahakamani kuwa upelelezi wa kesi ya kuomba rushwa ya dola za Marekani milioni
nne (zaidi ya Sh bilioni nane) inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Ephraim Mgawe, na wenzake haujakamilika.
Hayo yalidaiwa jana na Wakili wa Takukuru, Emmanuel Jacob
mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kesi hiyo ilipotajwa na kuangalia kama
upelelezi umekamilika.
Baada ya Jacob kudai kuwa upelelezi haujakamilika, Hakimu
alikubaliana na maelezo yao na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 18 itakapotajwa
tena. Mgawe anadaiwa kufanya kitendo hicho ili atoe zabuni ya ujenzi wa bomba
la kupakulia mafuta.
Mbali na Mgawe, vigogo wengine ni Mkurugenzi wa zamani wa
Uhandisi, Bakari Kilo (59), aliyekuwa Meneja wa Mazingira , Theophil Kimaro
(54) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DB Shapriya, Kishor Shapriya (60).
Jacob alidai kuwa tuhuma za kuomba rushwa zinawakabili
Mgawe, Kilo na Kimaro, ambao wanadaiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti
na maeneo tofauti ambayo hayafahamiki kati ya mwaka 2009 na 2012.
Ilidaiwa kuwa kwa kutumia nafasi zao, waliomba rushwa ya
dola hizo kupitia kwa wakala wa kampuni ya DB Shapriya kuiwezesha kampuni ya DB
Shapriya kupata zabuni ya ujenzi wa bomba la kupakulia mafuta kwenye rasi ya
Mji Mwema kinyume na sheria ya Takukuru.
Alidai walifanya hivyo ili Shapriya ashinde zabuni
iliyokuwa ikishindaniwa namba AE/0116/2008-2009/10/59.
0 comments:
Post a Comment