Fidelis Butahe
SIKU chache baada ya Rais John Magufuli
kuagiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), lizitimue wizara na taasisi zote
zinazodaiwa mamilioni ya kodi ya pango, kauli hiyo imezitetemesha wizara hizo
ambazo sasa zimelipa malimbikizo yanayofikia Sh. bilioni 8.
Jana NHC ilitangaza kupokea fedha hizo zilizolipwa
na taasisi za Serikali na watu binafsi, likieleza
zimeelekezwa katika ujenzi wa nyumba 300 za makazi mkoani Dodoma.
Malipo hayo yamefanyika baada ya agizo
la Rais John Magufuli alilolitoa Septemba 7 mwaka huu, kwa kuzitaka wizara zote
zinazodaiwa na shirika hilo kuwa zimelipa madeni hayo na zikishindwa ziondolewe
kama ilivyokuwa kwa kampuni ya Mbowe Hotels inayomilikiwa na mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe.
Katika orodha ya taasisi zilizolipa,
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na
Mazingira na Wizara ya Elimu ndio zimemaliza deni lote, huku Wizara ya Afya
ikilipa Sh 300,000 tu katika deni la Sh bilioni 1.4.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi
wa Utawala wa shirika hilo, Raymond Mndolwa, alisema taasisi za Serikali
zilikuwa zikidaiwa Sh bilioni 9.3 na watu binafsi Sh bilioni 4.
“Kulipwa kwa madeni haya ni miujiza kwa
kweli tunamshukuru Rais Magufuli. Sh bilioni 5.9 zimeshalipwa na taasisi za
Serikali zilizokuwa zikidaiwa na sasa deni limebaki Sh bilioni 3.3,” alisema
Alisema malipo hayo ni sehemu kidogo ya
idara na taasisi za serikali zilizopanga katika majengo ya shirika hilo na
kubainisha kuwa wameamua kupeleka kiasi hicho cha fedha katika ujenzi wa nyumba
eneo la Iyumbu, Dodoma kuunga mkono mpango wa Serikali kuhamia Dodoma.
“Ujenzi wa nyumba hizi tayari umeshaanza.
Kuna taasisi hazijalipa deni lote ila tumeingia makubaliano maalumu. Kama walikuwa
na deni la nyuma wataendelea kulilipa ila lile deni la kila mwezi ni lazima
lilipwe,” alisema Mndolwa.
“Tunaendelea kufuatilia deni ili na
tunaamini idara na taasisi husika zitamaliza deni ifikapo mwisho wa mwezi
Desemba.”
Kuhusu watu binafsi, Mndolwa alisema
licha ya baadhi kulipa, wapo ambao wanaendelea kulimbikiza madeni yao huku
akibainisha kuwa hivi karibuni watafanza zoezi kabambe la kuwaondoa wadaiwa
wote.
“Tutawaondoa katika majengo ya shirika
na kuuza samani kufidia deni wanalodaiwa, kuwatoa katika vyombo vya habari na
kuwapeleka mahakamani ili walipe deni,” alisema.
Alisema kati ya Sh bilioni 4 waliozokuwa
wakidaiwa watu binafsi, wamelipa Sh bilioni 2 tu na kwamba katika wilaya ya
Ilala wameondoa watu 40 katika majengo ya shirika hilo, zoezi ambalo
litafanyika Upanga, Temeke na Kinondoni.
“Kwa watu binafsi mazungumzo hakuna.
Haiwezekani tukudai Sh360,000 kwa mwezi na ushindwe kulipa mwaka mzima huku
ukiwa kimya. Tukikukuta tunakutoa nje,” alisisitiza.
Katika orodha ya wadaiwa hao, Wizara ya
Habari, licha ya kulipa Sh milioni 70, bado inadaiwa Sh bilioni 1.1, huku Wizara
ya Ujenzi ikilipa Sh bilioni 2.1 na kubakisha
deni la Sh milioni 58.
Ends
0 comments:
Post a Comment