Magufuli atikisa wakubwa duniani

Rais John Magufuli
*Ni wenye uwekezaji nchini wanaovuna bila kuacha faida
*Aanza na Barick ya Canada, sasa StarTimes ya China
*Mikataba mibovu yapanguliwa mmoja baada ya mwingine

Mwandishi Wetu


MSIMAMO wa Rais John Magufuli katika uteteaji rasilimali za Taifa kunufaisha wananchi, umeonekana kutisha wamiliki wa kampuni zinazovuna mali nchini kutoka nchi zilizoendelea.

Siku chache baada ya Rais kuhoji uwekezaji wa kampuni ya China ya StarTimes, kwenye Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa miaka saba bila kutoa hata senti, jana bosi wa kampuni hiyo alifika katika Shirika hilo kujaribu kurekebisha hali.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano uliorushwa moja kwa moja na TBC,  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Xinxing Pang amesafiri kutoka China kuja kujadiliana na Serikali baada ya kusikia msimamo wa Rais.

“Ameamua kuja kutoka China ili kujua moja kwa moja kuhusu msimamo wetu,” alisema Dk Mwakyembe ambaye aliweka wazi kuwa Serikali ilishafikia uamuzi wa kuchukua dhidi ya mkataba huo.

Itakumbukwa kuwa Mei 16 Rais Magufuli alifanya ziara ya kushitukiza TBC Mikocheni, Dar es Salaam, ambako pamoja na mambo mengine, alihoji sababu ya StarTimes kuendelea kuwapo, wakati imekuwa ikipata hasara kwa miaka saba sasa.

Kutokana na madai ya kampuni hiyo kupata hasara kwa miaka saba, Rais Magufuli alimwagiza Dk Mwakyembe kuchukua hatua stahiki kama mkataba huo hauna manufaa, kwa sababu haiwezekani kila wakati kampuni hiyo idai kupata hasara.

Akizungumza jana baada ya kumaliza kikao na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Dk Mwakyembe alisema baada ya agizo la Rais, walikaa na TBC, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wizara kupitia masuala mbalimbali ya StarTimes.

Baada ya mapitio hayo na mkutano wake wa jana na bosi wa kampuni hiyo ambapo StarTimes ilitoa sababu zake, Dk Mwakyembe alisema waliunda Kamati itakayofanyia kazi changamoto zilizoonekana za kukosa faida kwa miaka saba.

Alisema Kamati hiyo imeundwa na watu watano kutoka Tanzania na watano China, ambao wamepewa siku saba kutoa majibu.

“Suala hili hatutaki lichukue muda mrefu, tunataka liishe mwezi huu na uamuzi utakaofikiwa na Kamati nitampigia simu Mwenyekiti kumweleza. Kwa sababu tayari sisi tulikuwa na msimamo wetu,” alisema bila kuutaja.

Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, Kamati hiyo itaendelea na kazi wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad akitarajiwa kuwasilisha ripoti yake kuhusu biashara ya miaka saba ya StarTimes bila faida wakati wowote kuanzia jana.

“Tunataka jambo hili limalizike mapema, ndiyo maana tukaamua kushughulika kwanza na mkataba, na hiyo ripoti ya CAG itasaidia majadiliano yatakayopatikana kwenye Kamati na ndiyo maama tumeipa  siku saba tu,” alisema.

Mwenyekiti Xinxing alisema yuko nchini kwa sababu ya maswali kadhaa ya Rais Magufuli kuhusu kampuni yao, kwa hiyo wameyazingatia na watayafanyia kazi.

“Tunafanya juhudi ya kujibu maswali hayo na ndiyo maana nimekuja kuzungumza na Waziri na kutoa mrejesho wa kazi tulizofanya za StarMedia na pia tutaeleza sababu za kampuni yetu kutupa hasara na njia ya kutupa faida baadaye,” alisema.

StarTimes yenye mkataba na TBC, imekuwa ikiuza visimbuzi vya kurusha matangazo ya televisheni na kukusanya ada ya vipindi ya kila mwezi kutoka kwa wateja, huku ikidai haipati faida kwa mwaka wa saba sasa.

Barick

Ujio wa bosi huyo wa  StarTimes kutoka China, unafanana na wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold ya Canada, Profesa John Thornton, muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuzuia usafirishaji wa kontena 277 za mchanga wenye madini mchanganyiko ikiwamo dhahabu maarufu kama makinikia.

Profesa Thornton alifika baada ya Kamati ya Rais Kuchunguza Makinikia hayo kutaka kupitiwa upya kwa mikataba ya uchimbaji madini, ili uvunaji wa rasilimali hiyo, unufaishe Taifa.

Mikataba mingine

Mkataba wa StarTimes na TBC unajadiliwa, wakati Serikali imeanza mjadala wa kihistoria wa mikataba ya uchimbaji madini, huku ikiwa imefanikiwa kubadili mkataba mwingine wa uwekezaji uliokuwa ukituhumiwa kunyonya Taifa wa kampuni ya kimataifa ya kuhudumia shehena za kontena bandarini (TICTS).

Kampuni ya TICTS ilikuwa na mkataba na Serikali wa miaka 15 hadi mwaka 2025, ambapo Serikali ilikuwa ikipata kodi ya dola milioni saba tu kwa mwaka.

Rais Magufuli alipoingilia kati, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema kampuni hiyo ilikubali kuongeza kodi hadi dola milioni tisa kwa mwaka.

Profesa Mbarawa alisema Serikali iliendelea kushikilia msimamo kuwa kampuni hiyo iongeze kiwango hicho hadi dola milioni 12, lakini walikataa na kuondoka.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, baadaye kampuni hiyo ilikubali kuongeza kodi kutoka dola milioni saba hadi 14 jambo ambalo halijawahi kutokea miaka ya nyuma, na wakakubaliana bei itakuwa inapanda kwa asilimia 3.8 kwa mwaka.

Mbali na mkataba wa TICTS, ni katika awamu ya tano chini ya Rais Magufuli, Serikali ilifanikiwa kuirejesha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwenye miliki yake, baada ya kumilikiwa na kampuni ya Bharti Airtel of India kwa asilimia 35 katika mkataba uliokuwa ukilalamikiwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo