Grace Gurisha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeshindwa
kutoa uamuzi kama itafuta shtaka la mauaji dhidi ya mke wa marehemu bilionea
Erasto Msuya, Miriam Msuya (41) au la, anayeshtakiwa kumuua dada wa marehemu
huyo, Aneth ikianisha sababu za kushindwa kufanya hivyo.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Godfrey Mwambapa
aliahirisha kesi hiyo jana hadi Desemba 21 mwaka huu kwa sababu bado hajamaliza
kuandika uamuzi huo ambao umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara kutokana na sababu
mbalimbali za kimahakama.
Hatua hiyo imefikiwa na mahakama hiyo, baada ya Wakili wa
Miriam, Peter Kibatala kuwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Magreth
Bankika wa mahakama hiyo kuwa hati ya mashtaka ina kasoro na kuomba ifutwe, pia
akidai kuwa wateja wake waliteswa na polisi.
Mbali na Miriam, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni
mfanyabiashara wa Jiji la Arusha, Revocatus Muyela (40). Kibatala alidai pia
kuwa washtakiwa hao waliteswa na askari kabla ya kuchukuliwa maelezo ili wakiri
kuhusika na mauaji hayo.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Diana Lukondo alisema
hati ya mashtaka iliyokuwa mbele ya mahakama iko sahihi kwani ina sababu zote
za kuitwa hati ya mashtaka, hivyo hoja za Kibatala hazina mashiko.
Muyela aliunganishwa katika kesi hiyo, baada ya kukamatwa
na kubainika kuwa na yeye anatuhumiwa katika mauaji hayo.
Aneth alikuwa dada wa marehemu bilionea Msuya, alichinjwa
na watu wasioulikana nyumbani kwake Kibada, Block 16, Kigamboni, jijini Dar es
Salaam Mei 26, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment