Waandishi Wetu
WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ikianza
mwaka wake wa pili madarakani tangu ilipoingia Novemba 5 mwaka jana, wakuu
watano wa mikoa wametajwa kung’ara kati ya 26 wa mikoa ya Tanzania Bara.
Wakizungumza na JAMBO LEO kwa nyakati
tofauti kuhusu utendaji wa viongozi hao wanaomwakilisha Rais John Magufuli katika
ngazi ya mikoa, watu wa kada mbalimbali walitoa maoni yao na kuwataja majina na
mikoa wanapofanya kazi.
Wakuu wa mikoa waliotajwa kufanya vizuri
katika kipindi hicho ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Amos
Makalla (Mbeya), Antony Mtaka wa Simiyu.
Wengine ni Mrisho Gambo wa Arusha na
John Mongella wa Mwanza, wote wakiwa katika umri wa ujana.
Wakuu hao wa mikoa wa Serikali ya Awamu
ya Tano wametimiza miezi tisa tangu walipoteuliwa, huku kukiwa na kumbukumbu ya
amri tano walizopewa na Rais John Magufuli, wakati wakila kiapo Ikulu, Dar es
Salaam.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi aliteua wakuu
wa mikoa 26 Machi mwaka huu akisema: “Mnakwenda kufanya kazi kwa ajili ya
kutatua kero za wananchi. Hamuendi mikoani kutangaza siasa, mnakwenda kutimiza
wajibu wenu kwa ajili ya wananchi.”
Aliwataka wawakilishi wake hao wakuu
kupambana na ujambazi, kusimamia ilani ya uchaguzi ya CCM, kutatua kero za
wananchi, kuzuia vijana kucheza pool table na kusimamia utekelezaji wa elimu
bure.
Haikushangaza alipofanya mabadiliko ya
wakuu watatu wa mikoa, Juni 26 mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kujaza nafasi ya aliyekuwa
mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Anna Kilango ambaye uteuzi wake ulitenguliwa
kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo zoezi la kubaini watumishi hewa.
JAMBO LEO imetafuta maoni ya watu wa kada
mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa wakuu wa mikoa katika kipindi cha miezi
tisa.
Kabla ya kuteuliwa kwao, Rais alitaja
vigezo ambavyo angetumia kuwapima wakuu wa mikoa na wilaya, akiwataka
kuzingatia suala la upungufu wa madawati, upungufu wa chakula na migogoro ya
ardhi.
Wakuu hao wa wilaya walikula kiapo cha
kwanza mbele ya Rais na cha pili waliapa kwa pamoja kwa kutumia dakika nane,
baadaye walisaini hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, inayotolewa
na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Wakuu hao wa mikoa waliotajwa kufanya
vizuri katika kipindi hicho ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,
Amos Makalla (Mbeya), Antony Mataka (Simiyu), Mrisho Gambo (Arusha) na John
Mongella (Mwanza).
Ofisa Mtendaji wa Chama cha
Wafanyabiashara wenye viwanda na Wakulima (TCCIA) mkoani Mbeya, Emile Malinza
alisema: “Makalla ni mfano wa kuigwa ikilinganishwa na watangulzi wake. Amefanya
mabadiliko makubwa, hasa kwenye bei za bishaa na migogoro kati ya Serikali na
wafanyabiashara kuhusu kodi katika soko jipya.”
Alisema mkuu huyo wa mkoa pia
amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji. Katika miundombinu
hasa wilayani Rungwe waliokuwa wakipata shinda kuvuka mito kutokana na
kukosekana kwa madaraja pamoja na kuhakikisha waliopewa viwanda wanaviendeleza.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), Richard Mbunda alimtaja Mtaka kuwa kiongozi anayefanya kazi bila
kuingiza siasa.
Alisema chini ya utendaji wake amebuni mradi
wa ‘Mkoa mmoja, bidhaa moja’ lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi kujiingiza
katika miradi inayoweza kuwaingizia kipato, ikiwemo kuzalisha bidhaa zinazotoka
mkoani humo, jambo alilodai kuwa litasaidia kuwaongezea kipato wanancho hao.
“Mradi huu umekuwa ukitumika katika nchi
mbalimbali duniani ikiwemo Japan, akiendelea na utaratibu huu ni wazi kuwa
atafika mbali zaidi,” alisema Mbunda.
Gambo naye ametajwa katika orodha hiyo
licha ya kuitumikia nafasi hiyo kwa muda mfupi, huku kiongozi wa Nane Nane, Kanda
ya Kaskazini, Arthur Shayo alisema licha ya mkuu huyo wa mkoa ‘kupambana’ na
mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, bado ameweza kufanya mazuri.
“Kwa kweli ameweza kupambana na
unyanyasaji wa wafanyabiashara wadogo kwa kiasi kikubwa na kuondoa usumbufu kwa
wafanyabiashara kwa kupunguza mlundikano wa kodi,” alisema.
Mhadhiri mwingine wa Udsm, Dk Benson
Bana alisema: “Licha ya kulalamikiwa katika baadhi ya mambo, lakini Makonda amefanya
mengi mazuri. Hasa kuwafikia wananchi na kusikiliza kero zao.”
Alifafanua: “Amekuwa mbunifu zaidi, hasa
ule mpango wake wa upandaji miti ambao unaweza kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji
zuri zaidi.”
Huku akieleza jinsi Makonda alivyowatuhumu
makamanda wa polisi kwa rushwa amekuwa akishiriki katika ujenzi wa wodi za
hospitali mbalimbali mkoani humo.
Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika (NCU)
jijini Mwanza, Juma Mukilu alisema Mongela ni kiongozi aliyefanya mazuri mkoani
humo licha ya juzi agizo lake kuwaondoa wamachinga kupingwa na Rais Magufuli.
“Anashirikiana na wananchi katika ujenzi
wa barabara tena hata kwa kubeba mawe kwake ni sawa tu…, pia amekuwa bega kwa
bega na wakulima kwa kupanga bei za mazao ambazo wafanyabiashara watazimudu,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment