Celina Mathew
SERIKALI imesema saruji haijapanda na kufungwa
kwa kiwanda cha mfanyabiashara maarufu wa Nigeria, Alhaji Aliko Dangote, hakuwezi
kuathiri bei ya saruji.
Akizungumza na mwandishi wa JAMBO LEO jana
kwa simu, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema ni
vizuri pia ikaeleweka kuwa kupanda au kushuka kwa bei ya saruji, si ajabu bali
ni jambo la kawaida katika biashara, hata wakati kiwanda cha Dangote kilipokuwa
kikizalisha.
Waziri Mwijage alifafanua kuwa uwezo wa
kuzalisha saruji iliyosindikwa nchini ni tani milioni 10.3, inayozalishwa ni
tani milioni 7.1 na mahitaji ni tani milioni 4.3.
“Licha ya kuwapo maeneo ambayo saruji
imepanda, lakini kuna maeneo mengine imeshuka, ni suala la kawaida, maana hata
jana nilipiga simu Kagera kwa sasa mfuko ni Sh 16,000 na Bukoba Sh 16,000
wakati zamani ilikuwa Sh 22,000,” alisema.
Alisema saruji ipo ya kutosha na nchi
ina uwezo wa kuzalisha nyingi zaidi, hivyo kiwanda kimoja kikifungwa hakiwezi
kuathiri viwanda 11 vilivyobaki nchini, isipokuwa kitakachotokea ni kwa
wanaotumia saruji ya kiwanda hicho ndio wataathirika kwa kiasi kikubwa.
“Suala la kufungwa kwa kiwanda kimoja
haliwezi kuathiri vingine ila hapo watakaopata tabu ni wanaonunua na kutumia
saruji ya kiwanda hicho hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi,” alisema.
Katika hatua nyingine, alisema viwanda
vyote vinatumia makaa ya mawe ya nchini na uzalishaji wake kwa sasa ni tani
45,000 kwa mwezi.
Alifafanua, kuwa kwa kawaida mawe hayo
hayawezi kuzalishwa na kurundikwa, kwa kuwa wakati mwingine husababisha
milipuko, hivyo huzalishwa kulingana na maombi ya mtu au kiwanda.
“Makaa ya mawe ya nchini yana ubora na
viwango vilivyowekwa kwenye uzalishaji wake, hivyo yapo na yanapatikana kwa
wingi, kuna watu wameahidi kuongeza mashine za kuzalishia hivyo hata uzalishaji
wake utaongezeka,” alisema.
0 comments:
Post a Comment