Mary Mtuka
Dk Jakaya Kikwete |
SERIKALI imetoa onyo kali kwa Gazeti la
Mtanzania kwa ilichoeleza kuwa ni gazeti hilo kuandika habari zisizo za kweli
na zilizolenga kumdhalilisha Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
Mbali na onyo hilo kwa Mtanzania,
Serikali imesema haitasita kuvichukulia hatua kali za kisheria vyombo vya
habari vitakavyokiuka maadili na itaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo hivyo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
jana iliyosainiwa na Kaimu Msajili wa Magazeti, Patrick Kipangula, Serikali
ilisema Mtanzania toleo namba 8370 ya Novemba 20 na toleo 8372 la Novemba 22,
ilichapisha habari zenye vichwa vya habari,'JK azuiwa Uwanja wa Ndege' na Ukweli
Safari ya JK Uarabuni' zikieleza kukwama kwa msafara wake kwenye Uwanja wa Ndege
wa Kimatafa wa Mwalimu Julius Nyerere.
"Habari hizo si za kweli na
zililenga kumdhalilisha Rais mstaafu na familia yake, Serikali imesikitishwa na
jambo hilo, kwani zilipotosha umma wa Watanzania na kuacha wakijiuliza
maswali," alisema Kipangula na kuongeza:
“Kupitia uzito wa tuhuma za gazeti hilo
kwa kiongozi huyo mstaafu tunatoa onyo kali na endapo kitendo hicho kitajirudia
tena, basi hatua kali zitachukuliwa.”
Taarifa hiyo ilivikumbusha vyombo vya
habari kuzingatia maadili ya tasnia ya habari badala ya kuandika na kutangaza habari
zenye lengo la kutaka kugombanisha viongozi wastaafu na Serikali iliyoko
madarakani.
0 comments:
Post a Comment