Suleiman Msuya
January Makamba |
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira),
January Makamba, amesema anasikitishwa na uharibifu wa mazingira nchini aliouelezea
kuwa ni kizingiti cha maendeleo ya nchi.
Aidha, Makamba amesema Serikali iko kwenye
mchakato wa kutangaza maeneo nyeti ya mazingira katika mikoa ya Mbeya na Rukwa,
ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Makamba alisema hayo jana wakati
akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari nchini kuhusu ziara aliyofanya
kwenye mikoa tisa nchini.
Alisema jitihada za Serikali kukabiliana
na changamoto za umasikini na kukuza uchumi, zitafikiwa iwapo jamii itabadilika
na kutunza mazingira kwa kushirikiana na wadau.
Makamba alisema katika ziara aliyofanya
kwenye mikoa ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma
na Tabora, alibaini uharibifu mkubwa wa mazingira, hali ambayo inaweza kusababisha
janga kwa nchi.
Alisema Rukwa uharibifu mkubwa
umefanyika kwenye Ziwa Rukwa hali ambayo imesababisha viboko kuathirika zaidi.
Makamba alisema kwenye Mto Katuma ambao
ndio mhimili wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi, walihesabu michepuko 40 ambayo imesababisha
maji yasifike mbugani na hivyo kusababisha viboko na wanyama wengine kutaabika
na hata kufa.
Aidha, katika uharibifu wa misitu alisema
takwimu zinaonesha zaidi ya heka 1,000 zinakatwa miti kila siku ambapo kwa
mwaka zaidi heka 367, 000 zimekatwa.
"Hali ya uharibifu wa mazingira ni
mbaya, wapo watu wanakata hadi mininga kwa ajili ya kukausha tumbaku, nadhani
ni wakati wa kuamka kukabiliana na hali hii," alisema.
Makamba alisema wakataji miti wanaingia
katikati ya misitu na kukata, hali ambayo inasababisha wasimamizi kutotambua
haraka.
Alisema uharibifu upo pia kwenye
uchimbaji madini ambapo baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakitumia sumu na
kuathiri mazingira, wananchi na wanyama.
Alibainisha kuwa ng'ombe ni tatizo kubwa
katika uharibifu wa mazingira na kwamba wako kwenye mchakato wa kushirikisha
wadau na wizara zingine, ili kufikia mwafaka.
Alisema katika kukabiliana na hali hiyo,
wameelekeza milima ya Mbeya na Mto Rukwa kuwa maeneo nyeti ya mazingira, ambapo
Serikali itatangaza kwenye Gazeti la Serikali mapema mwakani.
Makamba alisema awali Mlima Mbeya
ulikuwa na vyanzo 50 vya maji, lakini kutokana na uharibifu wa mazingira vimebakia
vinne ambavyo ni vichache, jambo ambalo litachangia ukosefu wa maji kwa siku za
karibuni, kama hakuna hatua zitachukuliwa.
Alisema ameagiza kuandikwa sheria ndogo
za kusimamia mazingira vijijini, kuundwa kwa kamati, kufanyika tathmini za
athari za mazingira na kuitishwa kikao kikubwa cha wadau ili kujadili hali ya
mazingira.
Waziri alisema ameelekeza Shirika la Umoja
wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lihakikishe ndani ya mwaka mmoja,
liwezeshe wakimbizi kuacha kukata miti kwa ajili ya kuni na kufanya tathmini ya
athari ya mazingira.
Hali kadhalika alisema wameyapa maeneo
sita kipaumbele ili kukabiliana na hali hiyo ambayo ni uwepo wa NEMC, Ofisi ya
Makamu wa Rais na Halmashauri kujengewa uwezo, kupunguza matumizi ya mkaa na
kuimarisha uwezo wa taasisi.
Maeneo mengine ni kutafuta rasilimali,
kuweka msukumo mpya kwenye upandaji wa miti nchini na kuondoa matumizi ya
mifuko ya plastiki.
0 comments:
Post a Comment