Fidelis Butahe, Dodoma
MVUTANO umeibuka bungeni kati ya
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe na Naibu Spika, Dk Tulia
Ackson baada ya Mbunge huyo wa Hai kumwuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa swali
lililopingwa na Naibu Spika kwa maelezo kuwa ni la kisheria si la kisera.
Sakata hilo liliibuka asubuhi katika
kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, baada ya Mbowe kuhoji sababu za Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema kusota rumande kwa kukosa dhamana, Peter
Lijualikali wa Kilombero anayetumikia kifungo cha miezi sita gerezani na
wanachama wengine wa Chadema wanaokabiliwa na mashitaka mbalimbali.
Mbowe alimtaka kiongozi huyo wa shughuli
za Serikali bungeni, aeleze kama ni sera ya Serikali kuua vyama vya upinzani,
huku akisema Rais John Magufuli alipata kutamka kuwa atavimaliza vyama vya
upinzani kabla ya mwaka 2020.
Kwa maswali hayo, Dk Tulia alimtaka
Waziri Mkuu kujibu swali linalohusu sera na kuachana na yanayogusa masuala ya
kisheria.
Jambo hilo liliwafanya wabunge wa Upinzani
huku wakipiga meza kwa takribani dakika tano kupinga, wakimtaka Naibu Spika aache
Waziri Mkuu ajibu swali hilo.
Katika swali lake la msingi, Mbowe
alisema wakati jana ikiwa ni Siku ya Haki Duniani, imepita miezi mitatu tangu
Lema aanze kusota rumande huku akinyimwa dhamana licha ya kuwa iko wazi.
Pia alisema Lijualikali anatumikia kifungo
cha miezi sita jela kwa kosa la kisiasa sambamba mwenyekiti wa chama hicho wa mkoa
wa Lindi, Suleiman Mathew aliyefungwa miezi minane na madiwani zaidi ya sita na
viongozi wengine 215 nao wakifungwa au kuendelea na mashitaka huku zikifanyika
hila za kuidhoofisha CUF.
“Haya yanayoendelea katika Serikali
ambayo ni kinyume na utamaduni na mazoea yetu kama Taifa, je ni utekelezaji wa
sera ya kuua upinzani chini ya Rais Magufuli?” Alihoji Mbowe.
Kabla ya Waziri Mkuu kujibu swali hilo,
Dk Tulia aliingilia kati na hali kuwa hivi:
Dk
Tulia: Katika swali lako kuna masuala ya kisera na
kisheria. Maswali yanayomhusu Lema na Lijualikali na madiwani sita ni ya
kisheria, hayo kuhusu leo (jana) kuwa siku ya haki duniani, Waziri Mkuu anaweza
kuyajibu.
Majaliwa: Nakanusha, Rais hajawahi kutangaza kuvifuta vyama vya upinzani,
nchi inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu na kuna Bunge, Serikali na
Mahakama. Hakuna mhimili unaoingilia mhimili mwingine. Jambo lililopo
mahakamani halizungumzwi kokote, siwezi kuzungumzia hilo.
Mbowe: Kwa kuwa Rais anaonekana kuvunja Katiba ikiwa ni pamoja na kupiga
marufuku mikutano ya vyama vya siasa, je tukileta ushahidi kuwa Rais amekusudia
kuumaliza upinzani kabla ya 2020, Waziri Mkuu utakuwa tayari kuwajibika kwa
kujiuzulu?
Dk
Tulia: Mbowe swali lako la maelezo ya jumla, yako
sawasawa ila la kumtaka Waziri Mkuu kuwajibika si la kisera, kuwajibika si sera
uliza swali la kisera.
Mbowe: Labda swali langu nilielekeze kwa Naibu Spika (Dk Tulia). Swali
langu lilikuwa la mwendelezo ambalo hutokana na majibu ya msingi yaliyotokea.
Kama kulikuwa na msingi wa kisera kwenye swali la msingi, swali la mwendelezo
linakwenda kutokana na majibu yaliyotolewa. Waziri Mkuu aseme tu kama yupo
tayari kujiuzulu tukileta ushahidi.
Katika maelezo yake, Dk Tulia alitaka
Mbowe ajikite katika swali la kisera jambo ambalo Mwenyekiti huyo wa Chadema
alipinga na kusisitiza kuwa huenda mambo yanayofanyiwa wapinzani, wabunge,
mawaziri Serikali inayafurahia.
0 comments:
Post a Comment