Salha Mohamed
WATUMISHI wawili wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), wamekamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,
kwa madai ya kupitisha kemikali bashirifu.
Kemikali hizo ni aina ya ephedrine, ambazo
hutumika kutengezea dawa za kulevya aina ya heroin.
Kamishna wa Operesheni wa Mamlaka hiyo,
Mihayo Msikhela alisema jana Dar es Salaam, kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwenye
operesheni ya siku nne na wengine wawili wanasakwa na Mamlaka hiyo.
“Watumishi hawa wawili tayari tunao na
taratibu zinafuatwa na muda wowote watafikiswa mahakamani, bado wawili
tunaendelea kufuatilia nyendo zao,” alisema.
Alisema msako unaendelea nchi nzima dhidi
ya wakulima, waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya, za mashambani
na viwandani.
Kamishna Msikhela alisema dawa za
kulevya za mashambani ni kero kubwa nchini na kwamba walipokabidhiwa hati ya
watu wanaojihusisha na biashara hiyo, baadhi ya watuhumiwa walibainika kuwa
watumishi wa umma.
Msikhela alisema mikoa ya Tanzania Bara
imeonesha mafanikio makubwa katika kubaini na kuteketeza mashamba ya dawa za
kulevya aina ya bangi na mirungi.
Alitaja mkoa wa Tanga kuteketeza mirungi
kilo 44 na bangi puli tatu, Morogoro bangi kilo 18 na heroin kete tatu, Shinyanga
bangi kilo 10, Kagera ekari 14 za bangi na mirungi ekari moja.
Mikoa mingine ni Njombe bangi nusu
ekari, Songwe heroin kete 274 mirungi kilo tatu, Tabora bangi kilo sita,
Singida bangi misokoto 203 heroin kete moja.
Aliongeza kuwa mkoa wa Rukwa bangi kete
105, Mbeya bangi kilo tano, Kigoma bangi nusu ekari, Lindi bangi gramu 496 na
heroin kete 50.
Mkoa wa Simiyu uliteketeza bangi ekari
40, Ruvuma bangi gramu 300 na Tarime Rorya bangi ekari 36.
“Kati ya hii, mkoa uliofanya vizuri
zaidi katika ukamataji dawa za kulevya za mashambani ni Simiyu kwa kuteketeza
mashamba ya ekari 40,” alisema.
Alisema kwa dawa za viwandani, mkoa
uliofanikiwa kukamata dawa za kulevya nyingi ni Lindi iliyokamata kete 50 na unafanyika
utaratibu wa kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, huku watuhumiwa
wakiendelea kuhojiwa.
Alisema hadi sasa watuhumiwa
waliokamatwa kwa dawa za kulevya ni wengi huku akibainisha kuwa watalitolea
ufafanuzi.
Alipongeza wananchi waliotoa taarifa za
wauzaji na watumiaji dawa hizo akisema kunaonesha mafanikio huku akiwa na imani
ya Tanzania bila dawa za kulevya kuwezekana.
Aidha, Msikhela alipotakiwa kutaja
majina ya watumishi waliokamatwa alisema kutaja majina si sahihi.
Alipotakiwa kutaja orodha aliyokabidhiwa
kama kuna watoto wa vigogo au la, alisema: ” Naomba kukuhakikishieni kwamba
yeyote aliyetajwa kwenye orodha ataguswa hatutazami kigogo ni yupi na yupi si
kigogo yaliyomo mle ni majina ya wahalifu kama wahalifu wengine”.
Mbali na hilo, Mihayo alisema katika
orodha ya majina 97 waliyokabidhiwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda kama kuna waliokamatwa, alisema bado wanafuatilia na
watatoa taarifa.
Alipotakiwa kutofautisha kiutendaji kati
ya utajaji majina kwa awamu ya kwanza na ya pili, na hata ya tatu, alisema kutaja
na kutotaja yote ni mifumo ya uhakikishaji, kwamba makosa yanayosumbua mitaani
hayaendelei kusumbua tena.
Alisema yapo makosa ya wazi na
yaliyojificha, hivyo ya wazi itajulikana yako kwenye hatua ipi na yaliyojificha
hatua ipi na yanafuatiliwa kwa mfumo upi.
Aliulizwa endapo ikithibitika Makonda
hakufuata utaratibu wa kutaja majina kama atachukuliwa hatua, alishindwa kujibu
swali hilo huku akiwataka waulizaji kuangalia mifumo ya maswali ilivyo.
0 comments:
Post a Comment