Suleiman Msuya
Mwalimu Julius Nyerere |
KATIBU Mwenezi
wa zamani wa TANU na Mbunge mstaafu, Faustine Masha amesema ni vigumu katika
nchi ambazo zimeruhusu mifumo ya kidemokrasia kufanikisha Mfumo wa siasa ya Ujamaa
na Kujitegemea kwa kile alichodai kuwa hakuna uvumilivu wa kisiasa.
Aidha, Masha
ametoa siri ya siku nyingi kuwa iwapo watu wawili Mzee Daud Masasi na Balozi
Paul Rupia wasingekubali Azimio la Arusha lisingekuwepo kutokana na nguvu ya
kiuchumi ambayo walikuwa nayo wakati huo.
Masha aliyasema
hayo jana wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Azimio la Arusha iliyoandaliwa
na Kavazi la Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Alisema kwa
uelewa wake, Ujamaa na Kujitegemea ungeweza kufanikiwa iwapo nchi ingeendelea katika
mfumo wa chama kimoja, lakini kwa kuruhusu vyama vingi, falsafa hiyo itachukua
muda kueleweka.
Mbunge huyo wa zamani
alisema katika nchi ya kidemokrasia jamii inaishi kwa kukosoana hali ambayo
haina nafasi katika nchi za kijamaa.
Alisema viongozi
wakikosa uvumilivu wa kupokea kauli za kushutumiwa na kukosolewa ni wazi kuwa
hakutakuwa na misingi ya ujamaa.
"Mimi
ninavyoamini Azimio la Arusha lilijikita katika misingi ya ujamaa na
kujitegemea na wakati ule utekelezaji ulionekana lakini katika mfumo wa leo ni
vigumu kuona hilo likifanyika kwa sababu viongozi hawapo tayari umiliana,"
alisema.
Alisema mwalimu Nyerere
aliamini katika Ujamaa na Kujitegemea, akiamini kuwa ndio njia sahihi ya
kuchochea uzalishaji wa nchi na watu wake na si kutegemea watu wa nje.
Masha alisema ni
wazi kuwa kauli mbiu ya mhadhara huo kuwa 'ujamaa wa Mwalimu umezimuliwa au
umeteketezwa' kwa upande mmoja imeakisi uhalisia uliopo.
Katibu huyo
muenezi ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha UDP alisema
Azimio la Arusha haliwezi kurejea kwa kuwepo ni nia ya viongozi pekee bila
wananchi kuwa tayari.
Kuhusu uwezekano
wa Azimio kutopita iwapo Mzee Masasi na Rupia wasingekubali alisema hao ndio
baadhi ya Watanzania wachache ambao walikuwa na nguvu ya kifedha wakati nchi
imepata Uhuru.
Alisema iwapo
matajiri hao wangepinga ni wazi kuwa Azimio lisingepita na misingi ya ujamaa na
kujitegemea isingeonekana pia.
"Nakumbuka
siku ile kulikuwa na ajenda 11 lakini ajenda ya Azimio la Arusha ilichukua
kikao kizima lakini iwapo Masasi na Rupia wasingekubali hakuna kingeendelea ila
baada ya Mzee Masasi kuunga mkono maamuzi hata Rupia hakuzungumza tukajua hoja
imepita," alisema.
Alisema baada ya
makubaliano hayo kupita Februari 5 mwaka 1967 utekelezaji ulianza ikiwa ni
kutaifisha taasisi mbalimbali kama benki.
Masha alisema
utekelezaji ulifanyika haraka kupitia Mwalimu Nyerere na yeye akiwa muenezi wa
chama alifanikisha hilo kwa kufanya mikutano mbalimbali na kugawa vipeperushi.
Kwa upande wake
mtoa mada Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Makerere, Ahmed Mohiddin alisema
pamoja na changamoto zilizopo nchini Tanzania bado chembechembe za Azimio la
Arusha na misingi yake zipo nchini akitolea mfano umoja, ushirikiano na utawala
bora.
Alisema Nyerere
aliamini katika misingi ya umoja na ushirikiano kwa Bara lote la Afrika hali
ambayo ilichangia Tanzania kuheshimika duniani.
Prof alisema
katika nchi kama Kenya mfumo wa uongozi unatenga wananchi na viongozi hali
ambayo ni tofauti naTanzania.
"Mwalimu
alitamani Afrika iishi katika misingi ya utawala wa Afrika na si kuiga tawala
za nje ila hakueleweka hali ambayo inatutafuna hadi sasa," alisema.
Alisema katika
kumfuatilia Mwalimu aligundua kuwa ni kiongozi asiye mbinafsi hali ambayo
inagharimu viongozi wengi wa sasa.
Akichangia
katika mhadhara huo Mkuu wa wilaya mstaafu Charles Sotola alisema kutofanikiwa
kwa Azimio la Arusha kukichangiwa na viongozi kutolielewa.
Alisema viongozi
waliowengi kunzia ngazi za juu hawana uelewa hali ambayo inachangia waje na
mipango yao ambayo haitekelezeki.
"Baada ya
kustaafu kupitia chama cha wakuu wa wilaya wastaafu nilikuja kugundua kuwa sisi
ndio kikwazo katika mambo mengi ya maendeleo ikiwemo Azimio la Arusha,"
alisema.
Mwenyekiti wa
Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema Azimio la Arusha
lilikuwa na misingi ya kusaidia mshikamano wa watu hivyo ni vema kukawa na
mjadala wa pamoja ili kuirehesha nchi katika misingi hiyo.
Kwa upande wake
Richard Mabala alisema Azimio la Arusha lilitekelezwa na vijana wazalendo kama
Nyerere hivyo kutoa wito kwa Serikali kuwatumia ikiwemo kuwasikiliza
wanachotaka.
Akizungumzia
Azimio hilo Dickson Kamala alisema ni wakati wa kutenganishwa sasa na biashara
ili kuhakikisha kuwa heshima na utawala bora unakuwepo kama Mwalimu alivyotaka.
0 comments:
Post a Comment