Mwandishi Wetu
Profesa Mark Mwandosya |
Profesa Mwandosya ametajwa kuwa mmoja wa wazungumzaji
wakuu katika maadhimisho hayo ya yatakayofanyika jijini Dar es Salaam
yakihusisha mawaziri wa maji wa nchi 10 wanachama wa Bonde la Mto Nile, ambapo
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.
Ushiriki wa Profesa Mwandosya katika mkutano huo unatajwa
kuwa tukio la kwanza la hadhara tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015
alipojaribu kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini kura za
maoni hazikutosha.
Hivyo Profesa Mwandosya anatarajiwa kuvuta hisia za
wengi, hasa baada ya kukosekana kwenye majukwaa ya kisiasa na kijamii tangu
mwaka juzi.
Katika maadhimisho hayo, mambo mbalimbali yanatarajiwa
kujadiliwa ikiwamo umuhimu wa Mto Nile katika kuzipatia nchi wanachama maji,
chakula na umeme wa uhakika.
Mahitaji hayo yatatolewa kupitia miradi endelevu tofauti
inayofaidisha nchi wanachama kupitia rasilimali zake chini ya Taasisi
Inayosimamia Shughuli za Nile (NBI).
Naibu Mkurugenzi wa Maji katika Wizara ya Maji na
Umwagiliaji inayoandaa maadhimisho hayo, Sylvester Matemu alisema Profesa
Mwandosya amepewa nafasi hiyo kutokana na uzoefu wake na utaalamu katika sekta
ya maji.
Pia Matemu alisema Profesa Mwandosya amefanya utafiti na
kuandika kitabu kuhusu Mto Nile.
“Pamoja na Mwandosya, mawaziri wote wa maji kutoka nchi
wanachama watazungumza katika maadhimisho hayo ya kihistoria,” alisema Matemu
katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho hayo
mwishoni mwa wiki.
Alisema maadhimisho hayo yatafanyika Ukumbi wa Mikutano
wa Mwalimu Nyerere ukishuhudia pia upandaji miti, ambao utatanguliwa na
maandamano yatakayoanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa NBI, Mhandisi Innocent
Ntabana alisema madhimisho ya siku hiyo alitaja nchi wanachama kuwa ni
Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Sudan Kusini na Kongo.
Nyingine ni Ethiopia, Burundi, Rwanda na Misri ambapo
Ntabana alieleza kwamba maadhimisho hayo yatatumika pia kama jukwaa la
majadiliano kwa nchi hizo kuhusu rasilimali maji ya Mto Nile, mikakati ya
kuifanya endelevu na kukabili changamoto za kimazingira zilizopo ili liendelee
kuhudumia mamilioni ya watu wanaotegemea mto huo.
Profesa Mwandosya amekuwa kimya kwa zaidi ya mwaka mmoja
tangu kumalizika kwa mchakato wa kutafuta mgombea urais ndani ya CCM mwaka
2015, ambapo wagombea zaidi ya 35 akiwamo yeye walijitokeza na kuchujwa hatua
za awali.
Hali hiyo iliyozua malalamiko kutoka baadhi ya wajumbe
hata baadhi kuamua kujitoa CCM akiwamo Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa
aliyehamia Chadema.
Katika mchakato huo, Rais John Magufuli alipitishwa kabla
ya kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30 mwaka jana akimshinda mpizani
wake wa karibu, Lowassa.
Lowassa aliwania nafasi hiyo kupitita Chadema na kuungwa
mkono na vyama vinne vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa).
Mara kadhaa gazeti hili limekuwa likimtafuta Mwandosya
aliyewahi kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji katika Serikali ya Awamu ya Nne na
pia Waziri Asiye na Wizara Maalum ili kupata maoni yake kuhusu masuala mbalimbali
lakini mara azote simu yake imekuwa ikiita bila kupokelewa.
Ukimya wa Profesa Mwandosya ulizua maswali mengi, lakini
Desemba mwaka jana alipopigiwa simu na gazeti hili ili kuzungumzia pamoja na
mambo mengine mwaka mmoja wa Serikali ya Rais ya Awamu ya Tano na CCM, alisema
hana cha kusema.
“Mimi nipo kijijini kama unataka kujua masuala ya
kijijini kwangu niulize hayo ya mwaka mmoja wa Magufuli na CCM sina ‘coment’
kwa sasa nafanya shughuli zangu kijijini na kupumzika,” alisema.
Mwandosya anatajwa kama moja ya viongozi waliofanya kazi
kwa mafanikio huku akionesha utulivu na kujiamini kwa kila jambo hasa bungeni
ambapo alikuwa akitumia msemo wa kisomi kwa kuwataka wabunge watoe hoja na si
kufoka katika jambo wasilolijua.
0 comments:
Post a Comment