Edith Msuya
Bernard Konga |
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umepeleka
mapendekezo serikalini ya kutungwa sheria itakayotoa fursa kwa kila mwananchi
kuwa na bima ya afya.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
NHIF, Bernard Konga, alisema mapendekezo hayo yako serikalini na kinachosubiriwa
ni kukamilishwa taratibu, ili muswada ufikishwe bungeni.
Alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona wananchi
wengi hawana bima ya afya, hali inayosababisha baadhi yao kupata matatizo wanapopata
maradhi.
"Tunataka muswada huu ufike bungeni ili sheria ipitishwe
na kuwezesha asilimia kubwa ya wananchi kupata bima ili kuwapunguzia changamoto
za ugonjwa," alisema.
Alisema lengo la Serikali si kuwalazimisha wananchi, bali
kuwasaidia wapate huduma wanapopata matatizo na kuondokana kutegemea mtu mmoja mwenye
fedha.
Kwa mujibu wa Konga, ifikapo mwaka 2020 matarajio ni
kuhakikisha asilimia 85 ya Watanzania wanakuwa na bima ya afya.
"Serikali ina mtazamo mpana katika suala la afya
nchini na Mfuko umejizatiti kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya afya
kupitia mifuko yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo," alisema.
Konga alisema hadi Desemba mwaka jana wanufaika wa mifuko
hiyo ya NHIF na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), walikuwa asilimia 27 ya Watanzania
wote.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo aliasa wananchi wanaomiliki
bima kutompa mtu mwingine hata ndugu, kwani kumpa mwingine ni kosa la jinai.
"Si ruhusa kwa mwananchi mwenye bima, kumpa mwenzake
ni kinyume cha sheria na pia ni jinai," alisema.
0 comments:
Post a Comment