Mwandishi Wetu
Dk Hamis Kigwangalla |
NAIBU
Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla, ameagiza
hospitali zote za kanda, zianzishe vituo vya kutoa matibabu kwa waathirika na
dawa za kulevya ndani ya miezi sita kuanzia jana.
Akizungumza
katika kituo cha kuwahudumia watu wanaotibiwa ili kuachana na matumizi ya dawa
hizo kilichopo Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Dk Kigwangalla
alitoa maagizo mengine manne na kusisitiza kuwa wauza dawa hizo sasa wamebuni
mbinu mpya ya kuwarubuni walioacha kutumia.
Operesheni
ya kupambana na utumiaji na biashara ya dawa za kulevya nchini iliyoanza
takribani wiki tatu zilizopita, imeshika kasi na kusababisha dawa hizo kuwa
adimu mitaani, jambo lilosababisha waliokubuhu katika matumizi kupata athari na
kusaka matibabu katika vituo hivyo.
“Kituo
hiki kinatoa huduma kwa kuwapatia dawa za methadone. Nimefanya ziara hii kwa
sababu kuna ongezeko kubwa la wateja siku za hivi karibuni, kutokana na
kuongezeka udhibiti.
“Kuna
taarifa kwamba wanaouza dawa za kulevya wameathiriwa sana kwa kupoteza mapato
ya mabilioni ya fedha kwa uwepo wa vituo hivi, ambavyo kwa sasa vinahudumia
wateja 335, wameanza kubuni mbinu za kuwarudisha kwenye matumizi kwa mbinu
mbalimbali ikiwemo kudai kuwa methadone haifanyi kazi,” alisema.
Alisema
mbali na hospitali za kanda kuwa na vituo hivyo, hospitali zote za mikoa nchini
zinapaswa kuanzisha kliniki ya kutoa methadone ndani ya miezi sita.
“Pia alimuagiza Katibu Mkuu (Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), ahakikishe kuna daktari bingwa wa afya ya akili
kwenye kila mkoa, ili kuanzisha na kusimamia vituo vya kutoa tiba ya methadone.
“Mkurugenzi
wa halmashauri ya wilaya ya Kinondoni aongeze eneo la kliniki na watumishi
kwenye kituo hiki,” alisema.
Naibu
Waziri huyo alisema Kamishna wa Polisi wa Operesheni Maalum, naye anapaswa
kufuatilia wateja wanaotoka kliniki, ili kudhibiti mkakati wa wanaouza dawa za
kulevya, wanaolenga kuwarubuni na kuwarudisha kwenye matumizi baadhi ya watu
wanaotibiwa, ili kuachana na matumizi hayo.
Dk
Kigwangalla pia alitembelea kituo kama hicho kilichopo katika Hospitali ya
Temeke.
0 comments:
Post a Comment