Mwandishi Wetu
RAIS John Magufuli amekutana na Makamu
wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), anayeshughulikia nishati,
Amadou Hott aliye nchini kwa mazungumzo na wataalamu na viongozi, ili kuboresha
sekta ya nishati hususan umeme.
Taarifa ya Ikulu iliyotumwa jana kwa
vyombo vya habari, ilieleza kuwa Hott yuko nchini ikiwa ni utekelezaji wa
mazungumzo yaliyofanywa kati ya Rais Magufuli na Rais wa AfDB, Akinwumi Adesina
jijini Addis Ababa, Ethiopia Januari 31.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao
walikubaliana kuongeza ushirikiano kati ya AfDB na Tanzania katika maendeleo,
huku mkazo ukielekezwa katika kupata majawabu ya kuongeza uzalishaji umeme wa
gharama nafuu.
Hott alielezea kuguswa na dhamira ya Rais
Magufuli ya kuongeza uzalishaji umeme wa gharama nafuu, ili kufanikisha mipango
ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa viwanda na aliahidi Benki yake kuhakikisha
dhamira hiyo inafanikiwa.
Rais Magufuli alimhakikishia Hott kuwa
Serikali yake iko tayari kutoa ushirikiano wakati wowote itakapohitajika ili
kufanikisha dhamira hiyo.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alizungumza
na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini, Jean Mutamba Ikulu, Dar
es Salaam.
0 comments:
Post a Comment