Mwandishi Wetu
Viongozi wa Jukwaa la Wahariri |
KITUO cha Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini
mwa Tanzania (SAGCOT), kimewataka wahariri kuwa mstari wa mbele kuhamasisha
kilimo na kutangaza fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.
Rai hiyo ilitolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT,
Geoffrey Kirenga wakati akizungumza kwenye semina iliyoandaliwa mwisho mwa wiki
kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuwaeleza wanahabari shughuli
zinachofanywa na kituo hicho katika kuinua kipato cha wakulima wadogo.
“Katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania
ina fursa nyingi za kilimo lakini hazijafikiwa au kuchangamkiwa kutokana na
kukosa uthubutu,” alisema.
Kirenga aliongeza kuwa, “wanahabari mna nafasi nzuri
kuzitangaza fursa hizo kwa Watanzania kwa kutumia vyombo vyenu na kuhakikisha
sekta ya kilimo nchini inakua na kuinua kipato cha wakulima wadogo,”.
Alisema sekta ya kilimo ina fursa nyingi kwa maendeleo ya
Watanzania na Taifa kwa jumla huku akitoa mwito kwa wanahabari kuandika zaidi
habari zinazohusu sekta ya kilimo na fursa zake ili kuhamasisha Watanzania
wengi kujikita katika sekta hiyo.
Akitolea mfano kiwanda cha kukoboa mpunga kilichopo
Kilombero, alisema ni cha kwanza kwa ukubwa na ubora katika ukanda huu.
“ASAS ni kiwanda kinachoongoza kwa usindikazi maziwa
katika ukanda huu kwa siku kina uwezo wa kusindika lita 50,000 lakini wanapata
lita 20,000 tu kutoka kwa wafugaji,” alisema.
Alisema fursa hizo zinapotea na sababu kubwa ni ng’ombe
kukosa malisho bora na cha kushangaza Australia wanatumia nyasi za Tanzania
kulisha ng’ombe wao halafu wanakuja kutuuzia nyama na maziwa.
“Vilevile tuna tatizo la kuhifadhi chakula, mahindi
yanayozalishwa nchini kwa mwaka ni kati ya tani milioni sita hadi saba lakini
yanayohifadhiwa kwa njia za kisasa ni kati ya tani milioni moja hadi mbili,
yaliyobaki yanahifadhiwa kwa njia za kienyeji yanaishia kuharibika, ipo haja
serikali ikatengeneza maghala katika maeneo ya uzalishaji,” alisema Kirenga.
Akizungumzia malengo ya kuanzishwa mpango huo, Naibu
Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Jennifer Baarn alisema, “kazi yetu ni kama
madalali baina ya wakulima na serikali, tunaangalia matatizo yanayorudisha
nyuma sekta ya kilimo na kwa pamoja tunatafuta namna ya kuyatatua. Lengo ni
kuhakikisha mnyororo wa kuongeza thamani ya mazao unaleta tija kwa wakulima
hasa wadogo.”
Alisema wamejiwekea utaratibu ambapo kila mwaka
kunafanyika kongamano linalowakutanisha wadau wa kilimo ambao kwa pamoja
wanajadili njia sahihi za kufanikisha baadhi ya maazimio yaliyofikiwa mwaka
uliopita.
Naibu Ofisa huyo alisema kwa mwaka huu kongamano hilo
litafanyika mapema mwezi ujao jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa wahariri waliohudhuria semina hiyo kutoka
gazeti la Raia Mwema, Ezekiel Kamwaga alisema kwa sasa ipo haja wananchi
wakaelewa kuhusiana na kilimo kwa sababu shughuli hiyo ina kipato kikubwa.
“Yapo mengi niliyojifunza kwa hakika kilimo kinalipa,
kazi yetu wanahabari ni kuieleza jamii umuhimu wa kilimo na kazi hiyo
tutaifanya kwa weledi,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment