*Viko
maeneo wanakoishi vigogo kisiasa, kiuchumi
*Walalamikia
polisi kushiriki na ‘wazungu wa unga’
Enlesy
Mbegalo
Baadhi ya watuhumiwa mihadarati |
IKIWA ni siku ya pili tangu Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwapa siku 10 wenyeviti wa serikali za mitaa kutoa
taarifa za nyendo za wanaojihusisha na dawa za kulevya, wenyeviti hao wametaja
vijiwe mama vya uuzaji na utumiaji mitaani kwao.
Wenyeviti hao wa mitaa ya Oysterbay,
Kunduchi, Kawe na Magomeni, wamesema vita hivyo vinawezekana na wanachohitaji
ni ushirikiano zaidi kutoka Serikali Kuu, Polisi na Mkoa.
Baadhi ya wenyeviti hao walisema vita hivyo
vilikuwa vigumu kutokana na baadhi ya polisi wasio waaminifu kuchukua rushwa,
kujihusisha na uuzaji, kutumia dawa hizo na ‘kutembea’ na wasichana wanaojiuza kwa
kuwa baadhi yao hutumia na kuuza mihadarati hiyo.
Ukwamani
Mwenyekiti
wa Ukwamani, Sultani Jetta alisema mtaa wake
umekuwa ukitumika kwa uuzaji wa mihadarati na amekuwa akikemea mara kwa mara na
kutoa taarifa Polisi Kawe lakini wahusika wamekuwa wakikamatwa na kutolewa.
“Tamko la Mkuu wa Mkoa Makonda limekuja
kwa wakati mwafaka kwangu, kwani nimepambana sana na vita hivi, baada ya kuona
vijana wengi mtaani kwangu wanaangamia, ila sikuwahi kupata msaada zaidi ya
hawa watu kuwekwa ndani na baada ya siku tatu kutolewa,” alisema Jetta.
Alisema eneo maarufu ambalo limekuwa
likitumika ni la soko la zamani, ambalo ni maarufu sana kwa uuzaji na utumiaji
wa mihadarati hiyo.
“Kwa kuwa biashara ya dawa za kulevya
inahusisha baadhi ya askari na tayari kwenye kituo chetu cha Kawe kuna mmoja
wao amesimamishwa kazi kwa tuhuma hizo, hivyo imani yangu ni kwamba yawezekana
kuna wengine watajitokeza kupambana kinafiki ili kujisafisha wakati ni miongoni
mwao,” alisema Jetta.
Aliongeza: “Binafsi orodha
nilishaikabidhi muda mrefu kituo cha Kawe na hakuna jipya na orodha hiyo ya
majina nitaipeleka kwa Mkuu wa Mkoa kwa kuwa ameonesha nia ya
dhati ya kupambana.”
Alisema alipata kutoa taarifa kwenye
kituo hicho kuhusu polisi maarufu anayetuhumiwa kama kibaraka wa wauza ‘unga’
mara kwa mara kwenye kijiwe cha mtaa wake, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Nadiriki kusema baadhi ya askari wa
muda mrefu katika kituo cha Kawe ni vichaka vya wauza dawa za kulevya na
nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wazazi wa maeneo ya kijiwe hicho,
kwa jinsi wanavyopishana kupokea hongo,” alisema na kuongeza:
“Hivyo nawaomba wenyeviti wenzangu wa mkoa
huu, tuwe wakweli bila kuficha maana hili ni janga kwa vijana wetu.”
Kunduchi
Mwenyekiti
wa mtaa wa Kunduchi, Richard Rusisye alisema katika
mtaa wake, kuna vijiwe vya uuzaji na utumiaji dawa za kulevya yakiwamo maeneo ya
Meko Uwanja wa mpira, Kokoni na Pwani.
“Eneo la Kokoni ni ambalo linatumika na
watu wengi kutoka sehemu mbalimbali za Jiji na polisi wakienda kuwakamata
hukimbilia kwenye mikoko, kwani eneo hilo ni la mikoko,” alisema.
Rusisye alisema pia kuna baadhi ya baa
kwenye mtaa wake ambazo zimekuwa zikitumika kuuza na matumizi ya mihadarati
hiyo.
Oysterbay
Mwenyekiti wa mtaa wa Oysterbay, Zefrin Lubuva alisema ukanda wa Barabara ya
Haile Salassie ni kero kutokana na watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya, pia
baa bubu alizosema zinachangia kukithiri kwa biashara hiyo.
Lubuva alisema kabla ya tangazo la Serikali,
waliendesha operesheni mtaani kwake na kubaini watu kujificha kwenye biashara
ndogondogo ukiwamo uuzaji wa pombe za ‘viroba’.
“Tuko pamoja na Mkuu wa Mkoa kwenye vita
hivi vikubwa ambapo nguvukazi ya Taifa hili, vijana, wanaangamia huko na
tutatoa taarifa, kwani unakuta kuna watu wanafanya kazi za kung’arisha viatu,
kumbe wanajihusisha na biashara hizo,” alisema
Aliongeza: “Nimepiga marufuku biashara
ya ‘viroba’ kwenye mtaa wangu na uwepo wa bajaji.”
Mzimuni
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mzimuni, Hassan
Ngonyani alitaja maeneo yanayotumika kuuza na kutumia dawa za kulevya kuwa ni
Tanganyika Packers, Maringo, Mikoroshini, bustani za maua na karibu na ukuta wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kambi ya Lugalo.
Pia baadhi ya wenyeviti walisema vita
hivyo vinahitaji uthubutu wa hali ya juu, kwani ni vikubwa na vinajulikana na
baadhi ya polisi ambao wamekuwa wakichukua rushwa kwenye vijiwe hivyo.
“Maeneo mengi polisi wamekuwa wanafeli
kutokana na kupokea rushwa, kuuza, kutumia na kujenga urafiki na wauza
mihadarati,” alisema mmoja wa wenyeviti ambaye hakuwa tayarin kutaja jina lake.
Hata hivyo, baadhi yao walisema wameanza
kupokea simu kutoka kwa wahusika wakiwasihi wasiwataje itakapohitajika orodha
ya majina ya watumiaji na wauzaji mihadarati hiyo.
0 comments:
Post a Comment