Mwandishu Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema atamwagiza Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuchunguza ukusanyaji mapato ya
Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Alitoa kauli hiyo jana alipotembelea
makao makuu ya shirika hilo Dar es Salaam kwa lengo la kujionea mwenendo wa
uendeshaji wake.
“Nitamwagiza CAG aje aangalie mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya
shirika hili kuanzia mwaka jana lilipoanza kufanya kazi hadi sasa,” alisema.
Waziri Mkuu alisema
Serikali haiko tayari kuona shirika hilo linakufa tena, hivyo aliwataka
viongozi wake wahakikishe linaendeshwa kwa mafanikio kwa manufaa ya Taifa.
Pia aliwataka waache
kukusanya mapato kwa kutumia risiti za kuandika kwa mkono na badala yake waanze
kutumia mfumo wa elektroniki ili kuzuia upotevu wa mapato hayo.
“Vitu vingi vinavyokwenda
manual ni rahisi kufa. Serikali tumeagiza malipo yote yafanyike kielektroniki
na kote tunakotumia mfumo huu tumepata mafanikio,” alisema.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa ATCL, Witness
Mbaga ajiridhishe na fedha zinazokusanywa katika eneo la mizigo kama ziko
sahihi, lengo ni kudhibiti upotevu wa mapato.
Hata hivyo, Waziri Mkuu
alitaka viongozi wa shirika hilo kuhakikisha wanazingatia ratiba ya njia na
muda wa safari ili wasipoteze wateja.
0 comments:
Post a Comment