Mwandishi Wetu
Kamanda Charles Mkumbo |
JESHI la Polisi mkoani hapa limekanusha kuwashikilia
raia tisa wa kigeni waliodaiwa kughushi nyaraka za kuishi na kufanya kazi
nchini.
Badala yake Jeshi hilo kupitia Kamanda
wake wa Mkoa, Charles Mkumbo, limekiri kuhoji raia watatu wa kigeni ili kusaidia
ushahidi wa taarifa zilizolifikia Jeshi hilo na Idara ya Kazi mkoani hapa
kuhusu uhalali wa vibali vya raia hao kufanya kazi nchini.
Wageni hao ni wafanyakazi wa kampuni ya
uwindaji wa kitalii ya TGT ya Ngaramtoni mkoani hapa, ambayo imekuwa ikifanya
uwindaji huo tangu mwaka 1990.
Waliohojiwa na uraia wao kwenye mabano
ni Cliff Duvell Hunter (Afrika Kusini), Nana GrosseWoodley (Ujerumani) na
Nicolas Carel Stubbs (Afrika Kusini).
Kamanda Mkumbo alisema jana kwamba baada
ya kuwahoji waliwaacha kwani walifuata taratibu zote za kupata vibali hivyo,
ingawa baadaye viligunduliwa kuwa vya kughushi.
“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa
wageni hao walifuata utaratibu wote ikiwa ni pamoja na kulipa ada na tozo zinazotakiwa
lakini wakapewa vibali vya kughushi, tuliwahoji na kuwaacha,” alisema Mkumbo na
kuongeza:
“Inaonekana vibali hivyo vilighushiwa na
maofisa wa Serikali huku wageni wakiwa hawajui lolote, hivyo kwa unyeti wa
suala hilo, kikosikazi maalumu kinafuatilia ili kupata undani wake.”
Uchunguzi unaonesha kushikiliwa kwa maofisa
wawili wa uhamiaji kutoka Manyara, Juma Fakhi na mwingine wa TGT ambaye
hakutajwa jina kuhusu sakata hilo la vibali.
Kamanda Mkumbo alithibitisha kukamatwa
kwa maofisa hao kutokana na vibali hivyo tisa vilivyolipiwa dola 5,000 za Marekani.
Mkumbo alisema jalada la maofisa hao
liko kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusubiri maelekezo ya kisheria.
Mmoja wa wajumbe wa kikosikazi hicho,
ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema mchezo huo wa kughushi vibali umekithiri
mkoani hapa, huku maofisa Uhamiaji na wa Idara ya Kazi wakinyooshewa vidole
kuwa vinara wakuu.
“Tatizo hili limekithiri sana mkoani
hapa kutokana na kuwa na wageni wengi wafanyao kazi hapa. Wageni wanadanganywa
sana kwa kupewa vibali feki huku serikali ikikosa mamilini ya fedha za kigeni
kila mwaka…zinaishia mikononi mwa wajanja wachache, uchunguzi wetu utabaini
mengi,” alisema.
Aliishukuru TGT kwa kutoa ushirikiano wa
kutosha kwa kikosikazi hicho, akiamini hatua hiyo itachimbua mzizi wa tatizo
hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGT, Michelle
Allard alipotakiwa kuzungumzia kadhia hiyo kwa njia ya simu, alisema kwa sasa
hawezi kusema lolote hadi uchunguzi wa kikosikazi hicho utakapokuwa
umekamilika.
0 comments:
Post a Comment