Annastazia Maginga, Mwanza
Stephen Wasira |
WASIRA
hajakubali kushindwa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wapiga kura wanne,
Magambo Masato, Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagila, kukata rufaa mahakamani.
Wanne hao
wanapinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyompa ushindi wa ubunge wa Bunda
Mjini, Esther Bulaya (Chadema) dhidi ya Stephen Wasira (CCM) kwenye Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba mwaka juzi.
Mwaka jana Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, ilimthibitisha Bulaya kuwa mbunge halali wa
Jimbo la Bunda Mjini baada ya kumshinda Wasira kwa mara ya pili kwenye kesi
iliyofunguliwa kwa mara ya kwanza Novemba 19 mwaka juzi.
Akizungumza na
waandishi wa habari juzi ofisini kwake, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu
Mwanza, Francis Kabwe alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa Februari 20.
Kabwe alieleza
kuwa kwa mujibu wa Katiba mtu anayeshindwa mara ya mwisho kwenye Mahakama ya
Rufaa hatakuwa na namna nyingine zaidi ya kukubali kushindwa na kuheshimu
uamuzi wa Mahakama.
“Hapa ndipo mwisho,
atakayeshindwa lazima akubaliane na matokeo kwa maana ndiyo inakuwa mwisho
wa rufaa, hivyo Mheshimiwa (Wasira) hapa ikila kwake ndiyo utakuwa basi tena,
hakutakuwa na namna, itabidi ajipange kwa miaka mingine,” alisema Kabwe.
Kabwe alisema
kesi itakuwa chini ya jopo la majaji watatu; Ibrahimu, Mabrouk na Mwalija,
ambapo pia alisema wanaweza kubadilishwa kutokana na majukumu mengine ya
kikazi.
Awali kesi
hiyo ilipoanza kusikilizwa Novemba 2015 Mahakama kupitia Jaji Chocha
alimtangaza Bulaya kuwa mbunge halali na kueleza kuwa mlalamikaji namba
moja, Masato na wa pili, Matwiga, walikuwa watalii tu mahakamani hapo na si
walalamikaji.
Jaji huyo alianisha
msingi wa kesi hiyo ambayo awali ilitupiliwa mbali na Mahakama hiyo, kabla ya
Mahakama ya Rufaa kuirejesha kusikilizwa upya, Jaji Chocha alisema walalamikaji
waliomba kubatilishwa matokeo yaliyompa ushindi Bulaya, huku wakiomba kuhesabiwa
kura upya na Mahakama kuamuru kurudiwa upya kwa uchaguzi wa ubunge huo.
Hata hivyo,
katika uchaguzi huo, Msimamizi wake aliiambia Mahakama kuwa Wasira alipata kura
halali 19,126 huku Bulaya akipata 28,568.
0 comments:
Post a Comment