Fidelis Butahe, Dodoma
MBUNGE wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Msukuma, ametaka
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda achunguzwe kwa maelezo kuwa amepata
utajiri ndani ya muda mfupi, ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba kadhaa na kumiliki
magari ya kifahari.
Msukuma ambaye juzi alihoji vita dhidi ya biashara ya dawa
za kulevya iliyoanzishwa na Mkuu huyo wa Mkoa, akimtaka aanze kukamata
aliowapangisha nyumba za kuishi wanaotajwa kujihusisha na biashara hiyo, akihoji
sababu za mawaziri kushikwa kigugumizi kuzungumzia vita hivyo.
Akizungumza bungeni juzi baada ya kuomba Mwongozo wa
Spika, Msukuma alisema dalili za kumhisi mtu anayejishughulisha na biashara
hiyo ni mwenendo wake bila kujali wadhifa wake.
“Mwaka juzi Makonda alikuwa akiishi kwa Membe (Bernard-
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje). Amekuwa Mkuu wa Mkoa ndani ya mwaka mmoja,
lakini anatumia gari la Lexus la Sh milioni 400 tena linalotumia mafuta ya
petroli,” alisema Msukuma.
“Kama hiyo haitoshi, ofisi yake ya Dar es Salaam imekarabatiwa
kwa zaidi ya Sh milioni 400 bila kufuata utaratibu wa ununuzi wa umma, ana
magari Toyota V 8, amejenga maghorofa kwa mwaka mmoja, hivi ni akina nani hasa
wanaotakiwa kujadiliwa na kufanyiwa uchunguzi?” Aliendelea kuhoji.
Alisema wakati hayo yakiendelea, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Utawala Bora, Waziri wa Katiba na Sheria na wa Mambo ya Ndani ya Nchi
wamepigwa ganzi.
“Mnalifanya suala hili ni la Rais kuhangaika na Mkuu wa Mkoa.
Hata kama anachangiwa na wahisani, sheria ya maadili inatutaka anayetuchangia
tumtangaze, lini amewatangaza wanaomchangia fedha?” Alihoji.
“Naomba Mwongozo wako Naibu Spika, kama wengine wanaweza
kufanya mambo ya hovyo na wakawa na kinga na mawaziri wakapigwa ganzi, hawawezi
kufuatilia, utuelekeze tunataka Makonda achunguzwe mali alizonazo,” alisema.
Alisema haiwezekani ndani ya mwaka mmoja Mkuu wa Mkoa amudu
kununua magari ya bei kubwa sambamba na kutembelea nchi mbalimbali Ulaya na
Marekani.
“Wala si suala la kuogopa, niko tayari kuwasaidia
mawaziri na vyombo vya usalama tuwaoneshe, tukitaka kumaliza wauza dawa tuanze
na mizizi, tusishike matawi,” alisema.
Hata hivyo, Naibu Spika Dk Tulia Ackson alipangua
Mwongozo wa Mbunge huyo kwa maelezo kuwa alizungumza jambo ambalo ni kinyume na
kanuni za chombo hicho cha kutunga sheria.
“Umetoa maelezo mengi siwezi kuyarejea hapa, maana
nitakuwa kama natoa msisitizo jambo ambalo kanuni zetu zinakataza kwa
maana mambo aliyoyataja, yule mtu aliyemtaja na wengine waliohusika, kama jambo
alilolisema si sahihi wanaweza kuja bungeni,” alisema Dk Tulia.
“Kama msimamizi wa leo kanuni ya 68 (7) zinataka niombwe
Mwongozo kwa mambo yaliyotokea bungeni mapema, kwa kuwa lilitokea jana (juzi)
tumia kanuni nyingine kuleta hoja yako.”
0 comments:
Post a Comment