Suleiman Msuya
KITENDO cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda, kuwaonesha hadharani watoto wenye umri wa chini ya miaka
18 na kuwatangaza wameathirika na Ukimwi kimekosolewa kuwa kimewaongeza watoto
hao matatizo mengine.
Wanasheria na wabunge wametoa maoni hayo
baada ya Makonda juzi kuwaonyesha watoto hao hadharani akisema wameacha dawa za
kulevya huku mmojawapo akiathirika kwa Ukimwi.
Katika maoni yake, Mwanasheria James
Marenga alisema alichofanya Makonda si sawa kisheria, huku akitoa angalizo kwa
viongozi wengine kusoma sheria za nchi kabla ya kufanya mambo yao.
Marenga alisema baadhi ya vyombo vya
habari vinapaswa kupongezwa kwa kutambua changamoto hiyo na kuficha sura za
watoto hao.
Alisema ingawa sheria inaelekeza kuwa
iwapo kitendo kinachofanyika ni kwa faida ya mtoto inawezekana kuwaweka wazi,
lakini tukio la juzi ni kuongeza tatizo kwa watoto hao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,
Mbunge wa Viti Maalumu na Mujumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Suzan
Lyimo alisema kitendo hicho ni kinyume na sheria ya mtoto na kimethibitisha, kwamba
Makonda hatoshi kwenye nafasi aliyonayo kwa kuwaongeza matatizo watoto hao na
kuwadhalilisha.
Lyimo alisema sheria ya mtoto iko wazi
kuhusu haki za mtoto hivyo anasikitishwa mtu aliyeapa kulinda Katiba anaivunja
kwa makusudi.
“Kimsingi Makonda hatoshi katika nafasi
aliyomo, nadhani hata katika ngazi ya ukuu wa wilaya alionesha kufeli, kilichopo
ni kubebana, ndiyo maana kila siku anaibuka na mambo yanayokwenda kinyume na
taratibu,” alisema.
Alisema kitendo cha kuwaonesha watoto
hao hadharani kinahatarisha maisha yao, kwani upo uwezekano wa kuwa alikuwa na
mpenzi na hakumwambia kuwa ameathirika hivyo kumdhuru.
Mbunge huyo alisema halikadhalika
kitendo hicho kimeweka mazingira mabaya kwa watoto hao kwa miaka ijayo, kwani
inaweza kuwa sababu ya kunyanyapaliwa.
Alisema yeye akiwa mjumbe wa Kamati ya
Bunge ya Huduma za Jamii, atahakikisha kitendo hicho kinajadiliwa Bunge lijalo
ili kuweka mambo sawa.
Mbunge Viti Maalumu, Anatropia Theonest (Chadema),
aliungana na Lyimo kuwa kitendo hicho kinaongeza tatizo lingine kwa watoto hao.
“Kiuhalisia watoto hao wako kwenye
matatizo ambayo yaliwapata wakiwa wadogo, halafu mtu mwingine kwa sababu ya
kutafuta sifa anawaongeza tatizo, akiamini ndiyo njia sahihi ya kuwasaidia
kumbe anapotea,” alisema.
Alisema viongozi kama Makonda ni janga
kwa Serikali, hivyo hakuna sababu ya kuwavumilia kwani wanahatarisha usalama wa
watu na nchi.
Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema ni
wakati wa wasimamia haki kushikamana ili kukomboa Taifa kwa alichodai ni
upungufu mwingi na ukiukwaji wa haki za watoto.
Mwenyekiti wa Bodi ya Jukwaa la Katiba
Tanzania (Jukita), Deus Kibamba alisema Makonda anajitahidi kufanya watu waache
kujadili hoja za nchi na kumjadili mtu, jambo ambalo si sahihi.
Alisema zipo sheria zaidi ya tano ambazo
zinaelekeza nini kifanyike kwa watoto kama wale, hivyo ni bahati mbaya kuna wakuu
wa mikoa ambao wanavunja sheria na Katiba na si kuilinda.
“Inaniuma kukaa kujadili sokomoko ambalo
analileta Makonda katika nchi kwa udhaifu wake wa kutojua sheria na Katiba au
labda anafanya hivyo ili aonekane,” alisema.
0 comments:
Post a Comment