Enlesy Mbegalo
Dk Yamungu Kayandabila |
KATIBU wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Dk Yamungu Kayandabila, ametoa siku 14 kwa wadaiwa sugu
kulipa kodi ya pango ya Sh milioni 220, ikiwamo Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji
kwa Mauzo ya Nje (EPZA) ambayo inadaiwa Sh milioni 144.
Nyingine ni hoteli ya Lamada ambayo
inadaiwa Sh milioni 54 na Tanganyika Motors ambayo inadaiwa Sh milioni 22.
Akizungumza na viongozi wa kampuni hizo
Dar es Salaam jana, katika oparesheni
maalumu ya kukusanya kodi ya pango la ardhi kutoka kwa wadaiwa sugu wa kampuni,
mashirika ya umma na watu binafsi kwa kuwafuata katika maeneo yao alisema
yasipolipwa mali zao zitapigwa mnada.
“Katika hatua ya kwanza Wizara kwa
kushirikiana na manispaa za mkoa wa Dar es Salaam imetoa notisi kwa wadaiwa
sugu wa kodi ya pango la ardhi,” alisema Dk Kayandabila.
Pia alisema Serikali kwa kutumia kampuni
ya udalali ya Msolopa Investment, itaendeleza oparesheni kwa kufika katika
ofisi za wamiliki wa viwanja na mashamba makubwa katika maeneo mbalimbali
nchini.
Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2016/17 Wizara ilipanga kukusanya Sh bilioni 111.77 kutokana na kodi ya pango la ardhi.
Alisema Wizara haitafanikisha malengo hayo endapo itaendelea kuwaachia wadaiwa sugu wasiotaka kulipa kodi.
0 comments:
Post a Comment