*Atajwa kukiuka haki kutangaza majina bila uthibitisho
*Sasa
asubiriwa na wabunge kujieleza kuhusu kauli zake
Leonce Zimbandu
Paul Makonda |
SIKU chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda, kutaja watuhumiwa 65 katika vita dhidi ya dawa za
kulevya, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema haki zimekiukwa
katika utajaji majina.
Mbali na LHRC baadhi ya wanaharakati
wameungana na kituo hicho kukosoa utaratibu uliotumiwa na Makonda.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi
wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kutangaza majina ya watu kwa
kuwahusisha na dawa za kulevya bila uchunguzi, ni kinyume na haki za binadamu na kuchafua majina yao kwa
vile hakuna uthibitisho wa kuwahusisha
na tuhuma hizo.
Alisema hayo baada ya mwandishi wa
habari hizi kumtaka azungumzie mazingira ya kutaja majina ya watuhumiwa kwa
kulinganisha na misingi ya haki za binadamu.
Dk Bisimba alisema majina ya watu yalipaswa
kutajwa kama Jeshi la Polisi nchini lingefanya uchunguzi wa awali na kupata
uthibitisho na Mahakama ndiyo yenye
jukumu la kutoa haki kwa kutafsiri sheria na si kiongozi.
“Kama uchunguzi wa awali ungefanyika,
suala la kutaja majina lingekuwa sahihi,
lakini kutangaza bila upelelezi ni
kinyume na sheria,” alisema.
Alisema Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema walipata
kupokea majina ya uongo, hivyo ni hatari kutangaza jina la uongo kisheria.
Wakili wa Kujitegemea, Nassor Kitugulu
alisema ni jambo la kushangaza mtu kutaja mbinu za adui, hiyo ni dalili kuwa
vita hiyo ni ngumu bila ushirikiano.
Alisema iwapo Serikali imedhamiria
kupambana na dawa za kulevya nchini baada ya kutambua njia zinazotumiwa,
ilipaswa kuweka mitego ya kunasa watuhumiwa.
“Tunajua kuwa dawa za kulevya zinapoteza
nguvukazi, lakini utaratibu wa kutangaza bila uthibitisho wa tuhuma ni kuchafua
sifa ya mtu kwenye jamii,” alisema.
Naye Fidelis Butahe anaripoti kutoka
Dodoma, kwamba Bunge juzi usiku liliweka historia kwa kupitisha maazimo manne,
yakiwamo ya kumtaka Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti
kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na ikibainika
wana makosa mamlaka zao za uteuzi ziwawajibishe.
Wateule hao wa Rais wanadaiwa kutoa
kauli za kudharau Bunge takribani siku tatu zilizopita na kuamsha hisia za
wabunge waliotoa kauli za kuwakemea bungeni.
Kwa sakata hilo, Mbunge wa Ukonga, Mwita
Waitara (Chadema) aliwasilisha hoja ya kutaka washughulikiwe, ambayo
ilijadiliwa kuanzia saa 1.30 usiku hadi saa 2.15 usiku na kuungwa mkono na
wabunge wote, wakiwamo mawaziri kwa kusema “ndiyo”.
Wakati wa mjadala wa hoja hiyo, Mbunge
wa Bunda, Esther Bulaya (Chadema) alieleza jinsi Makonda alivyompigia simu
kumweleza kuwa atawashughulikia wabunge, kwa sababu yuko karibu na ‘Bwana
mkubwa’, huku Joseph Msukuma (Geita Mjini-CCM) akitangaza vita na Mkuu huyo wa
mkoa.
Ilikuwa kama sinema bungeni, kutokana na
wawakilishi hao wa wananchi kuonekana kama wabunge wa chama kimoja, walipotoa
hoja zao kupinga kauli hizo, huku Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge
akiwaongoza kufuata kanuni za chombo hicho katika mjadala huo.
Maazimio hao ni; Makonda na Mnyeti
kuitwa mbele ya Kamati, Waziri wa Tamisemi kutoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa
na wilaya namna ya kufanya kazi zao bila kuingilia mihimili mingine.
Pia, mamlaka nyingine zikimhitaji Mbunge
kwa mashitaka ya aina yoyote lazima zimjulishe Spika wa Bunge na mamlaka ya
kinidhamu kuwawajibisha wateule hao wa Rais ikibainika wametenda kosa la
kudharau chombo hicho.
Ilivyokuwa
Akiwasilisha hoja hiyo usiku baada ya
kipindi cha asubuhi kutoruhusiwa na Chenge kwa maelezo kuwa alitaka
kujiridhisha kama Mbunge huyo alizingatia kanuni, Waitara alisema Mnyeti
ameonekana katika mitandao ya kijamii akisema wabunge hawajielewi.
“Haya mambo ndiyo yamejirudia wakati
nikiangalia televisheni ya Clouds, Makonda akionekana akisema sisi humu bungeni
tunasinzia,” alisema Waitara.
Alibainisha kuwa kwa mujibu wa Katiba
ibara ya 63(2), Bunge ndicho chombo kikuu kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na
kuishauri Serikali na linapitisha bajeti inayotumiwa na wateule hao wa Rais.
Alisema si sawa kwa wakuu wa mikoa na
wilaya kuwaweka rumande wabunge, madiwani na watumishi wa Serikali.
“Bunge linaingia katika majaribu makubwa
ya kudharauliwa. Tunakula kiapo humu, tuamue kwa niaba ya Watanzania, lakini
Mkuu wa Wilaya anasema hawa ni wapuuzi na Mkuu wa Mkoa anasema hawa wanalala
tu,” alisema.
Baada ya hoja hiyo, Waitara alitaka
ijadiliwe na Bunge na kutoa maazimio ili kurejesha heshima ya chombo hicho,
hoja ambayo Chenge aliipokea na kutoa nafasi kwa wabunge wanne, kujadili
kutokana na ufupi wa muda.
Mbunge wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu
alisema: “Nimehuzunika sana wabunge
tunafika mahali tunadharauliwa, halafu watu tunaangalia tu. Haya ambayo
yametokea kwa Makonda na Arumeru, pia yametokea Manispaa ya Dodoma. Mkurugenzi
anaongea na wabunge kama watoto.
“Mimi nadhani hata ile sheria ya
Marekani wenzetu wanaoteuliwa kwa ngazi za juu lazima wapelekwe bungeni, hapa
kwetu ingefaa kuletwa ili watu wa aina hii tuweze kuwamaliza hapa hapa. Wapo
wanaodhani wako juu yetu.”
Alisema ni jambo la hatari kujenga
Serikali yenye kiburi na kusisitiza: “Unapotaka kutoa pepo halibembelezwi.
Unataka kupunga majini huwezi kubembeleza. Lazima ukazane kupunga jini litoke.
Hatuwezi kutoa pepo kwa lugha nyepesi nyepesi (akipunguza sauti) pepo toka,
haiwezekani. Kama ni pepo tulikemee litoke.”
Bulaya alibainisha jinsi Makonda
alivyompigia simu na kutamba kushughulikia wabunge kwa kuwa yeye yuko karibu na
‘Bwana mkubwa’, huku akisisitiza kuwa Mkuu huyo wa Mkoa hakutengezwa kuwa
kiongozi.
“Makonda alinipigia simu na kunitisha
kwamba yeye yuko karibu na Bwana mkubwa, atatushughulikia wabunge. Alisema
ataanza na Msukuma, Halima Mdee (Kawe-Chadema), Esther Matiko (Tarime
Mjini-Chadema), Sugu (Joseph Mbilinyi-Chadema Mbeya Mjini) na Msigwa (Mchungaji
Peter-Iringa Mjini-Chadema),” alisema.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea
alisema: “Ni lazima heshima ya Bunge ilindwe kwa gharama yoyote. Makonda
anawapigia simu wabunge akitaja mmoja wa mawaziri kuwa ndiye anatuma wabunge
wamtukane.”
Naye Msukuma alisema haiwezekani Makonda
afanye kazi ya polisi na kuhoji aliko Mkuu wa Jeshi la Polisi, makamanda na
makamishna wake.
“Makonda ni nani katika hii nchi? Kama
Jairo (David-aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini) alitoka kwa
azimio la Bunge, Makonda ni nani? Mimi niko tayari kupambana na Makonda,”
alisema Msukuma.
Hoja hiyo pia ilitolewa ufafanuzi na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Waziri Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista
Mhagama, wakitaka wahusika hao wasikilizwe kwanza na kuachia ngazi zingine iwapo
watabainika kutenda kosa.
Chenge
Baada ya wabunge kuchangia, Chenge
alitoa nafasi kwa Waitara ambaye alihitimisha hoja hiyo na kutoa maazimio manne
ambayo Mwenyekiti huyo wa Bunge aliyafafanua na kupitishwa.
“Ni kwamba Waziri wa Tamisemi atoe
waraka kwa wahusika (wakuu wa mikoa na wilaya) kuwaeleza namna ya utekelezaji
wa majukumu yao. Pili, wahusika waitwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka
ya Bunge,” alisema Chenge.
“Endapo itaridhika, baada ya Kamati
kuwasilisha taarifa bungeni na Bunge kuridhia kwamba kuna jinai, hasa sheria
yetu ya Bunge inatoa madaraka kwa AG kufuatilia na vyombo vingine vya Dola,”
alisema Chenge.
Alisisitiza: “Sisi hatuwezi kufika huko
tunaishia katika haya yatakayoletwa na Kamati na suala la uwajibikaji
linakwenda sambamba na hayo yatakayoletwa na Kamati.”
Alipolihoji Bunge kama linakubaliana na
hoja hiyo, hali ilikuwa hivi; “mnaokubali hoja hii semeni ndiyo.” Wabunge wote
waliitika “ndiyo” na aliposema wasiokubaliana na hoja hiyo waseme “siyo”. Bunge
lilibaki kimya.
0 comments:
Post a Comment