…JPM akomelea vita vya mihadarati


Suleiman Msuya

Rais John Magufuli
“HAKUNA umaarufu kwenye mapambano dhidi ya matumizi ya  na dawa za kulevya.”

Hiyo ni kauli ya Rais John Magufuli jana, siku moja baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye kuzungumza na waandishi wa habari kupinga utaratibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutaja majina ya wasanii, akiwatuhumu kwa dawa hizo.

Nape alitaka busara itumike katika kuwakamata na kuwataja wasanii maarufu ili kuepuka kuwaharibia majina waliyojijengea baada ya kazi yao ya muda mrefu.

Kauli ya Nape ilitokana na hatua ya Makonda kutaja majina ya baadhi ya wasanii maarufu wa muziki na waigizaji nchini akiwamo Wema Sepetu kuwa wanajihusisha na mihadarati.

Lakini jana wakati akizungumza jana Ikulu, Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema vita hivyo havina kisingizio chochote kinachosababisha mtu aachwe kwa sababu ya umaarufu wake.

Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, alikuwa akiapisha wateule wake wanane akiwamo Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo.

Pamoja na Jenerali Mabeyo wengine walioapishwa ni Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali James Mwakibolwa, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dk Juma Malewa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz.

Wengine ni Katibu wa Tume ya Utumishi, Nyakimura Mhoji, Balozi wa Tanzania nchini DR Congo, Paul Meela na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Samwel Shelukindo.

Rais Magufuli alisema ni jukumu la kila kiongozi wa chombo cha usalama kushirikiana na wasaidizi wake kupambana na dawa za kulevya na isitokee mtu akaachwa kwa kisingizo cha umaarufu, cheo, uanasiasa, uwaziri, mtoto wa kiongozi au mke wa kiongozi na kwamba hata kama ni mkewe (Jannet) akihusika Polisi imkamate.

Alisema haingii akilini atokee mtu atetee wauza dawa za kulevya ambao wanatekeza kizazi ambacho ni nguvukazi ya Taifa.

Rais Magufuli alisema Lindi kuna tajiri analindwa licha ya kuwapo ushahidi wa kutosha wa biashara hiyo na kumtaka Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kusimamia mchakato huo kwa haki.

Alisema katika jambo la kushangaza, mtu huyo wa Lindi ana watu wakubwa wanaomtetea jambo ambalo si jema, kwa kuwa haiwezekani watu wadogo wafungwe huku wakubwa wakibaki mitaani.

“Napenda kutumia nafasi hii kukupongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu kwa hatua uliyochukua ya kuwasimamisha kazi watumishi walio chini ya mamlaka yako, kwani usingefanya hivyo, leo usingekuwa IGP,” alisema.

Alisema ni wakati wa vyombo vya ulinzi kuongeza nguvu bila kuonea mtu huruma na kuhakikisha wahusika wote wa biashara hiyo wanakamatwa, ili utaratibu wa kisheria uweze kufanyika.

Rais Magufuli alivitaka vyombo hivyo kuhakikisha kuwa operesheni hiyo inafanyika huku wakimtanguliza Mungu ili kuepuka kuonea mtu.

“Hivi ni vita vikubwa Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo naomba mwongeze ushirikiano kwani bila hivyo hatuwezi kufanikiwa,” alisema.

Alisema kizazi kinachoathirika kutokana na matumizi ya dawa hizo kingeweza kusaidia nguvu kazi ya nchi na kuchochea maendeleo.

Aidha, Rais alisisitiza Mahakama kutochelewesha kesi zenye   ushahidi dhahiri kuhusu dawa za kulevya, ili kuhakikisha wahusika wanatumikia kifungo.

Hadi jana Polisi ilishakamata watu 112 wanaotuhumiwa kuhusika na dawa za kulevya na uchunguzi ulikuwa bado unaendelea.

Akizungumza juzi na waandishi Dodoma, Nape alisema ni makosa kuwahukumu moja kwa moja kuwa wanajihusisha na biashara hiyo.

Alisema licha ya kuunga mkono juhudi za kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya, busara inapaswa kutumika  kuwabaini kwa sababu bado ni watuhimiwa.

“Ni muhimu kulinda haki ya mtuhumiwa, jambo lenye mjadala ni busara inayotumika kushughulika na wahusika ili kusaidia vyombo vingine kutaja wanaosambaza,” alisema.

“Tusiwahukumu kwa tuhuma maana wasanii kujenga brand (umaarufu) ni kazi kubwa ili kubomoa jina, ni sekunde tu. Ni sawa na kusema huyu kichaa, lazima jamii itamchukulia ndivyo sivyo.”

Februari 2, Makonda alitaja wasanii kadhaa pamoja na askari polisi 12 kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.

Mpaka sasa takribani wasanii saba wameshahojiwa huku askari hao wakisimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi yao.

Wasanii wanaochunguzwa kwa tuhuma hizo pamoja na Wema ni Khalid Mohamed (TID), Dogo Hamidu, msanii wa filamu nchini na Babuu wa Kitaa ambaye pia ni mtangazaji wa Televisheni ya Clouds.

Wengine ambao walitakiwa kufika kituo kikuu cha Polisi kuhojiwa jana ni wasanii Vanessa Mdee na Tunda Sabasita.

Tangu kuibuka kwa sakata hilo, wadau wamekuwa wakikosoa utaratibu uliotumika kwa maelezo kuwa wasanii hao wanahukumiwa kabla ya uchunguzi kufanyika ili ibainike kama wanajihusisha na biashara hiyo ama la.

“Ni vizuri tukaangalia tunalifanya katika namna ya kumlinda mtuhumiwa ili hata kama hausiki jina lake lisiporomoke,” alisema Nape.

“Matumizi ya dawa za kulevya yanaathiri wadau wetu ndiyo maana tumekuwa tukifanya juhudi za kuwasaidia kuwapeleka katika vituo maalumu vya kuwasaidia kuondokana na matumizi ya dawa hizi.”

Mbunge huyo wa Mtama alisema licha ya juhudi za kupambana na dawa za kulevya, kumekuwa na sintofahamu kuhusu sheria ya dawa za kulevya kutosema chochote kwa anayetumia.

Alisema wapo watu wa kada mbalimbali wanaotumia dawa za kulevya, lakini wasanii wanaonekana zaidi kwa kuwa ni maarufu na kubainisha jinsi Serikali kupitia wizara yake inavyowasaidia kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya, akiwamo msanii Rehema Chalamila ‘Ray C’.

“Matumizi ya dawa za kulevya ni tatizo la jamii nzima, mapambano lazima yaanzie kwenye familia zetu. Hawa watu wanahitaji msaada kama ilivyo kwa wagonjwa wengine,” alisema Nape.

Alipoulizwa nini suluhisho la utaratibu unaotumika kuwataja na kuwahusisha moja kwa moja wasanii na biashara hiyo alisema, “tuache jamii ijadili.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo