Suleiman Msuya
Rais John Magufuli |
RAIS John Magufuli amekabidhi kwa Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa mzigo wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Baada ya kukabidhiwa jukumu hilo, Majaliwa
alitaja wizara saba zitakazoshiriki moja kwa moja katika mapambano hayo.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache
baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuanzisha operesheni ya
kudhibiti dawa hizo.
Magufuli pia amekabidhi mapambano hayo
kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers
Sianga na viongozi wengine wanaohusika akiwataka kutoogopa mtu katika vita
hivyo.
Alizungumza hayo jana Ikulu baada ya
kuwaapisha wateule wake akiwamo Kamishna wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na
Dawa za Kulevya na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, mabalozi na
watendaji wengine.
“Waziri Mkuu nipo nyuma yako katika
mapambano haya naomba uongeze mapambano usiogope mtu kwa sababu ya uwezo, sura,
dini au jambo lolote,” alisema.
Rais Magufuli amepiga marufuku kiongozi au
mtumishi umma kuhangaika na utetezi au kutoa msaada kwa Watanzania waliohukumiwa
kifungo cha maisha au kunyongwa katika nchi mbalimbali duniani.
Alisema mapambano hayo ni vita vikubwa
hivyo ni jukumu la Waziri Mkuu na watu wake kuhakikisha wanasimama imara
kukabiliana nalo kwa maslahi ya Watanzania.
Alisema eneo hilo linakabiliwa na
changamoto nyingi huku akikiri kuwa hadi alipofanya uteuzi wa kamishna wa tume
hiyo hakuwa na taarifa kuwa anapaswa kufanya hivyo bali amemteua kutokana na
vyombo vyake na kwamba vyombo husika havikumpa jina.
“Lakini kusema ukweli sikujua kuwa
ninapaswa kuteua kamshina naamini hata Waziri Mkuu hakujua kuwa yeye ni
Mwenyekiti wa Baraza la Kupambana na Dawa za Kulevya, walimficha,” alisema.
Alisema iwapo sheria isingeelekeza Waziri
Mkuu kuwa mwenyekiti wa baraza hilo nafasi hiyo angechukua yeye ili kuhakikisha
mapambano yanakuwa makubwa na kumtaka Majaliwa kutorudi nyuma.
Alisema hata mawaziri wanaopaswa kuwa
wajumbe wa Baraza hilo hawakujua hali aliyosema inasababishwa na wasaidizi hao
kutotoa taarifa.
Rais Magufuli alisema pamoja na kuwepo
kwa sheria nzuri ya kupambana na dawa za kulevya, jitihada za kukabiliana na
hali hiyo zimekuwa za kuisuasua.
Alisema mapambano hayo ni ya watumishi
wote wa Serikali na kuwa kama yupo asiyetaka Serikali ifanye kazi yake ni vema
akapeleka mapendekezo bungeni ili kufanya mabadiliko.
“Suala la dawa za kulevya lisiangalie
cheo cha mtu hata kama akiwa kiongozi wa CCM. Aachwe afe mwenyewe kwani
hakutumwa na chama,” alisema na kuongeza:
“Wapo vijana wengi wanaoathirika na dawa
ya kulevya hivyo ni jambo la ajabu kama mtu atatetewa kwa kuwa ni kiongozi wa
CCM. Hiyo haitakubalika na mimi nikigundua sitamvumilia.”
Alisema Serikali ina mambo mengi ya
muhimu ya kufanya ila kwa sasa itahakikisha inapambana na dawa za kulevya
popote bila kumuonea mtu.
“Niwaombe Watanzania hii ni vita kubwa,
hivyo hakuna sababu yoyote ya suala hili kulifanya kwa mzaha kwani ni athari
kwa nchi katika uchumi,”alisema.
Atoa
onyo
Kuhusu Watanzania waliohukumiwa na kutuhumiwa
kuuza dawa za kulevya ughaibuni, alisema hadi sasa taarifa zinaonesha wapo 1,007
katika nchi mbalimbali na kuzitaka mamlaka husika kuwaacha wanyongwe.
Alisema hakuna Serikali inayoweza
kutetea watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, Waziri wa Mambo ya Nje na
mabalozi, waacheni wapate haki yao.
“Kama mtu ameshikwa katika nchi yoyote
ambayo sheria zake ni kunyonga muache anyongwe, nasema hili kwa dhati simung’unyi
maneno kwani tukicheka cheka Taifa letu litaangamia muwaache wanyongwe,” alisema.
Alisema kesi za dawa za kulevya nchini
ni nyingi ambapo alibainisha kuwa Dar es Salaam pekee zipo kesi 50 na kuvitaka
vyombo vyote vinavyohusika kushiriki kikamilifu kuhakikisha wanashinda kesi
hata kama si kwa asilimia 100.
Rais alisema Watanzania hao 1,007
wamegawanyika katika nchi mbalimbali ambazo ni Msumbiji (20), Nepal (4), Iran (63),
India (26), China (265) na 68 wamehumiwa kunyongwa.
Pia Brazili wapo (120), Uturuki (38), Ugiriki
(25) Afrika Kusini (269), Malaysia na Thailand (16), Indonesia
(1), Comoro (3), Nigeria (1), Kenya (66),
Uganda (15), Ghana (1), UIngereza (24), Japan (6) na wengine wengi.
Kamishna
wa Uhamiaji
Akizungumzia Idara ya Uhamiaji, Rais
Magufuli alimtaka Kamishina Jenerali Dk. Makakala kufanya mabadiliko makubwa
ndani ya idara hiyo kwa kile alichodai wapo watu wanajiona wao ni kila kitu.
Alisema uamuzi wa kumteua mwanamke
umezingatia uwajibikaji wake na kuwa alichokuwa anakifanya chuo cha uhamiaji aoneshe
kwa vitendo aliyokuwa anayafundisha.
Rais Magufuli alisema wapo watu ambao
wamekaa katika Idara lakini wamekuwa wakifanya mambo ambayo yanaenda kinyume cha
utumishi.
“Mfano wa hivi karibuni tulipokea wageni
wa asili ya Asia (Mabohora) zaidi ya 32,000 lakini hadi leo naulizia mapato ya
visa hakuna taarifa nataka uanze na idara ya fedha kuifanyia mabadiliko,”
alisema.
Alimtaka Kamishna Jenerali huyo
kuhakikisha utaratibu wa kutoa hati ya kusafiria kiholela unadhibitiwa pamoja
na uraia kwani inasababisha idara hiyo kushindwa kuwa chanzo cha mapato.
Mabalozi
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli
amewataka mabalozi wote aliyowateua kuiwakilisha nchi katika nyanja zote
kuchochea uchumi na uwekezaji.
Majaliwa
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri
Mkuu alisema mapambano dhidi ya dawa za kulevya ndiyo yameanza huku akiwapongeza
wakuu wa mikoa ambao wameonesha kuanza kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema kupitia mawaziri wa wizara
takriban saba anaamini jitihada zilizoanzishwa zinatapata nguvu, huku
akisisitiza kutoonewa mtu yeyote katika mapambano hayo.
Majaliwa alisema ni wajibu wa vyombo vya
dola kusimamia haki katika kukabiliana na hali hiyo kwani kutofanya hivyo
inaweza kuwa sababu ya kuingia kwenye migogoro isiyo na sababu.
“Nasisitiza kuwa tumejipanga kukabiliana
na hali hiyo ndiyo maana nimekuja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
ambaye atasimamia usafirishaji na mawasiliano, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia Wazee na Watoto, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.
“Nyingine ni Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Mambo ya Ndani na Mambo ya Nje ambazo
kwa pamoja zitatusaidia kukabiliana na hali hii,” alisema.
Kamishna
wa dawa za kulevya
Kwa upande wake, Kamishna Sianga alisema
amejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kupambana
na hali hiyo.
Alisema atahakikisha makundi mbalimbali
yaliyoathirika yanapata tiba na huduma ya elimu ya kuelewa madhara kama njia ya
kukabiliana kwa hatua ya awali.
Sianga alisema kipaumbele chake ni
kukabiliana na biashara ya bangi na mirungi ambazo zinapatikana nchini kabla ya
kuongeza nguvu katika dawa ambazo zinatoka nje.
Kamishna
wa uhamiaji
Kwa upande wake, Dk. Makakala alisema
amejipanga vilivyo kukabiliana na changamoto ambazo Rais amezianzisha huku
akisisitiza ushirikiano zaidi kwa watumishi wenzake.
Wengine walioapishwa jana ni Balozi wa
Tanzania nchini Algeria, Omar Yusuph Mzee, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji,
Joseph Sokoine na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgovano.
0 comments:
Post a Comment