Frankius Cleophace, Tarime
Mzee Nyamhanga Suguta darasani |
BAADA ya kusumbuliwa na hesabu ya chenji ya mauzo ya
ndizi kwa wateja wake, Mzee Nyamhanga Gesaba (78) mkazi wa kitongoji cha Kibeyo
kijijini Getenga wilayani hapa amejiunga na darasa la kwanza kujifunza kusoma,
kuandika na kuhesabu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, mzee huyo
alisema hakubahatika kwenda shule kwa sababu wazazi wake hawakumpeleka ingawa
alipenda elimu.
Alisema alianza shule ya awali mwaka jana kabla ya shule anayosoma
sasa kufunguliwa rasmi na Serikali.
Akifafanua sababu ya kuanza shule, Gesaba alisema amekuwa
akipata shida kurudishia wateja wake chenji katika biashara yake ya ndizi
anayofanya hivyo ili kuondokana adha hiyo ndipo akachukua uamuzi huo.
“Nikienda Tarime Mjini nashindwa kuongea Kiswahili, hivyo
nimeamua kusoma hapa, ili nielewe Zaidi, nawaheshimu walimu wangu pia nawapenda
wanafunzi wenzangu, lazima nitimize ndoto zangu licha na kuchelewa kusoma,”
alisema.
Riziki Focus ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msngi Makerero anakosoma
mzee huyo, alisema licha ya mwanafunzi
huyo kusoma, hatakuwa kwenye mfumo rasmi wa Serikali.
Hata hivyo, alisema wanasubiri Serikali ianzishe mfumo
rasmi wa masomo ya watu wazima kwenye shule hiyo ili wamsajili rasmi.
“Mwaka jana alishakuwa mwanafunzi kabla ya kufunguliwa
rasmi shule hii, lakini hakuwa kwenye mfumo rasmi endapo Serikali itaanzisha
Idara ya Elimu ya Watu Wazima tutamsajili aendelee na masomo, lakini kwa sasa
anafanya vizuri kwa sababu ameanza kuelea kuandika herufi,” alisema Mwalimu
Mkuu.
Mwalimu wa Darasa analosoma mzee huyo, Magreth Albinus
alisema alianza shule ya awali mwaka jana na amekuwa akifanya kazi zote shuleni
hapo ikiwa ni pamoja na adhabu zinazotolewa bila kujali umri wake.
Ofisa Elimu ya Msingi wa Halmashauri ya Wilaya, Emmanuel
Johnson alisema mbali na mfumo rasmi, upo usio rasmi ambao unaruhusu mwananchi
yeyote ambaye hakubahatika kupata elimu basi aipate nje ya mfumo huo.
Akasema pia kuwa kwa umri wa mzee huyo anaruhusiwa kujifunza
mpaka ajue kusoma na kuandika na baadaye aendelee na shughuli zake.
0 comments:
Post a Comment