Salha Mohamed
ASILIMIA 100 ya vijiji vinatarajiwa
kunufaika na nishati ya umeme ifikapo 2030.
Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Nishati
Vijijini (Rea), Boniface Gissima, alisema hayo jana katika taarifa yake kuhusu utekelezaji
wa shughuli za Wakala huyo za usambazaji wa umeme katika vijiji 7,873 Tanzania
Bara.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Awamu ya Tatu
ya mradi wa kusambaza umeme itatekelezwa katika vijiji hivyo kwa kipindi cha
miaka mitano kuanzia mwaka huu wa fedha hadi 2020/2021.
“Kati ya vijiji hivyo, vijiji 7,697
vitapelekewa umeme wa gridi na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi na utekelezaji
wake utajumuisha kuongeza wigo wa miundombinu ya usambazaji umeme,” alisema.
Alisema katika utekelezaji wa kuongeza
wigo wa miundombinu ya usambazaji umeme, tayari umeanza baada ya kusainiwa kwa
mkataba wa miradi hiyo Desemba mwaka jana katika mikoa sita itakayogharimu dola
za Marekani milioni 27.
Alisema mradi wa usambazaji wa vijiji 305,
utagharamiwa kwa fedha kutoka serikali ya Tanzania na Norway.
Gissima alisema ili kufikisha umeme katika
vijiji 3,559 ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme wa gridi, Serikali
inatarajiwa kutumia Sh. Bilioni 733.98.
“Katika miundombinu hii, mradi
utatekelezwa katika muda wa miezi 24 kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 hadi
2017/2018. Taratibu za ununuzi zinaendelea na wakandarasi wataanza kazi Aprili
mwaka huu,”alisema.
Alisema hadi sasa vijiji 4,395 kati ya
vijiji 12,268 sawa na asilimia 36, wameunganishwa na huduma ya umeme na hadi kukamilika
kwa mradi huo, vijiji 7,934 sawa na asilimia 65 vitakuwa vimefikiwa na mradi
huo.
Gissima alisema vijiji vitakavyosalia,
vitapelekewa umeme mwaka wa fedha 2018/2019 hadi 2020/2021 kadri upatikanaji wa
fedha utakavyoruhusu.
Katika hatu nyingine, Gissima alisema dola
za Marekani milioni 84, zimetengwa kwa ajili ya mradi wa kusambaza nishati jadidifu
kwenye maeneo yaliyombali na gridi na visiwa vilivyo kwenye maziwa na Bahari ya
Hindi.
“Katika mradi huu, dola milioni 42
zimetolewa na Benki ya Dunia, ambapo wakala ilitangaza Awamu ya Kwanza ya mradi
Septemba 23, mwaka jana na awamu ya pili itatangazwa April mwaka huu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment