Sharifa Marira na Charles James
WASOMI wametoa maoni tofauti kuhusu CCM
kuadhimisha miaka 40 ya kuzaliwa bila Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli na
wenyeviti wastaafu kuwapo, wakisema hatua hiyo si nzuri kwa ustawi wa chama hicho
tawala hasa kwa sasa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania (OUT), Salim Hamad alisema suala hilo limeacha maswali mengi kutokana
na kwamba si kawaida viongozi wakubwa kutohudhuria sherehe muhimu kama hiyo,
ambayo pia hutumika kama njia ya kujenga chama na mambo mbalimbali hutokea
wakati huo.
Alisema tatizo lililopo ni kwamba Dk
Magufuli ni mtendaji, si mwanasiasa
hivyo anajaribu kufanya utendaji zaidi ili wananchi waiamini CCM na
badala yake ameachia wasaidizi wake wafanye kazi .
“Ikiwa viongozi hao wameshindwa
kuhudhuria sherehe za chama kwa sababu ya kubana matumizi si njia sahihi, kwani
sherehe hizo si anasa ni njia ya kujenga chama na mara nyingi masikio ya Watanzania
huwa kwenye eneo ambalo sherehe hufanyika,’’ alisema Hamad.
Profesa Benson Bana, kutoka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) alisema hali hiyo ni moja ya maboresho ambayo
Mwenyekiti amekuwa akiyapigia kelele, inaonesha kuwa CCM ya sasa si ya matamko
na matamshi.
“Sera ya Magufuli ni kubana matumizi, anaonesha vitendo si maneno na hiyo ndiyo CCM
tuliyokuwa tunaitaka sherehe zinaweza kuwepo kwa njia yoyote ile, hata kwa
kwenda shamba au kuhamasisha jambo zuri kwa jamii na zikafanyika vizuri Zaidi,’’alisema
Profesa Bana.
Richard Mbunda alisema hakukuwa na
maandalizi maalumu ya kuitangaza siku hiyo, matangazo ya kawaida yaliyozoeleka
ya kuitangaza siku hiyo ya CCM hayakuwepo na ndiyo maana yameadhimishwa
kimyakimya na hii imetokana na hali ya kisiasa ilivyo nchini, imesababisha kukosa
msisimko kwa baadhi ya viongozi ndani ya chama.
Mbunda alisema sera ya Mwenyekiti wa chama
hicho kubana matumizi inaweza kuwa sababu nyingine ya kutoshuhudia viongozi
wakuu kuhudhuria maadhimisho hayo, kwani gharama zingekuwa ni kubwa zaidi
tofauti na kuwakilishwa na viongozi wa chini.
“Ni wazi zile shamrashamra zimepotea na
kutohudhuriwa huku kwa viongozi wakubwa kunaweza kuleta tafsiri hasi kwa
wapenzi na wanachama ambao wanaweza kuhisi pengine viongozi wanasusa chama
chao,” alisema Mbunda.
Ghamaly John ambaye ni msomi wa Chuo
Kikuu cha Mwalimu Nyerere alisema kutohudhuriwa huko kwa Rais Magufuli kunaweza
kuwa ni mwendelezo wa staili yake ya kutofanya kazi kwa mazoea, kama ambavyo
alionesha kwenye sherehe za Mapinduzi mwaka huu.
“Unajua Rais Magufuli amekuwa akionesha
kwamba yeye si mtu wa kufanya kazi kwa mazoea ya miaka iliyopita, hivyo
tusishangae akaibukia mkoa mwingine na kuadhimisha kwa staili ya aina yake.
“Lakini pia inatilia mkazo sera yake ya
kubana matumizi ambapo kama angehudhuria yeye na Shein (Dk Ali Mohamed - Rais
wa Zanzibar) pamoja na ujumbe wao gharama ingekuwa kubwa zaidi ikiwamo ya matangazo,”
alisema Ghamaly.
0 comments:
Post a Comment