*Ashangaa Mwanasheria Mkuu, DPP kuvutana
*Aitaka
Mahakama kusimamia kesi kwa weledi
Suleiman Msuya
Rais John Magufuli |
“LEO nawapa makavumakavu.” Hiyon ni
kauli ya Rais John Magufuli alipozungumza jana na familia ya wanasheria katika
maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika Dar es Salaam.
Rais aliamua kufunguka akitumia kauli
yake ya Msema Kweli ni Mpenzi wa Mungu akizungumzia uozo ndani ya Mhimili wa Mahakama,
lakini pia katika Wizara ya Sheria na Katiba.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli
aliweka bayana mgogoro ulio katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
George Masaju na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Biswalo Mganga bila kupatiwa
ufumbuzi.
Aidha, aliitaka Mahakama kufanya kazi
kwa weledi bila kupendelea, kwani kufanya hivyo kunasababisha wananchi kukosa
imani na chombo hicho akitolea mfano mahakimu 28 waliokuwa wakituhumiwa kuachwa
huru na sakata la Escrow.
Alisema yapo mambo mengi ambayo
wanayasikia na amekuwa akiyanyamazia, lakini inafikia mahali inamlazimu aseme
kutokana na ‘madudu’ yanayofanyika.
Rais alisema inashangaza viongozi hao
ambao kiasili wanatoka mkoa mmoja (Mara) kila siku wanalumbana jambo ambalo
linasikitisha na kushangaza.
“Tunayasikia, ni mengi katika ofisi ya
AG na DPP, ofisi hizi zinagombana zenyewe kwa zenyewe, nani hajui nawaulizeni
nani hajui hapa, nasema uongo jamani, Waziri unafahamu kwamba kuna mgogoro
katika ofisi hizo mbili na kwamba wanatoka mkoa mmoja na inawezekana wilaya
moja,” alisema.
Magufuli alisema waziri, DPP na AG wanapaswa
kukutana na kupata mwafaka ili mambo yaweze kwenda na kwamba wote ni wateule wa
Rais, hivyo kama ni masuala la kasma wazungumze na atangaalia njia ya kutatua,
kwani utaratibu unamruhusu.
Alisema mgogoro unaweza kuwa sababu ya
Serikali kushindwa kila kesi ambayo inafunguliwa, kwa sababu wahusika wa
kutetea hawako pamoja, hali inayosababisha majaji kuahirisha kesi kila siku kwa
kuamini kuwa wahusika watatambua tatizo.
Aidha, alisema eneo lingine lenye changamoto
ni Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwani
hawafanyi upelelezi huku wakiwa na ushahidi wa jambo husika.
“IGP upo hapa, leo nawapa tu zote
kavukavu haiwezeni umemshika mtu na pembe za ndovu, dawa za kulevya waziwazi halafu
unasema upelelezi haujakamilika unataka ukamilikeje?” Alihoji.
Rais alisema kudai upelelezi unafanyika kumesababisha
wakati mwingine ushahidi kupotea na mhusika kutoingizwa hatiani.
Alisema katika mazingira hayo ya vyombo
husika kuchelewesha upelelezi inafikia mahali dawa za kulevya kubadilishwa na
kuwa mihogo (unga) kutoka Sumbawanga, hivyo Mkemia kukosa ushahidi.
TLS
Akizungumzia Chama cha Wanasheria wa
Tanganyika (TLS) alikitaka kiache kuwa na mrengo wa kisiasa ili kusaidia nchi na
kuweka bayana kuwa hatateua wakili wa chama hicho kama kitakuwa na mrengo huo.
Alisema ana taarifa za baadhi ya
wanachama kushabikia siasa na kuwa wapo wanaotarajia kugombea uongozi.
“TLS imekuwa kama chama cha siasa na
hata hivi sasa kuna kampeni za watu kutoka chama fulani kutaka kukurithi wewe,
naamini kuwa mnatakiwa kuangalia maslahi ya nchi kwa kuwa watu wa kati kwa
maendeleo ya nchi,” alisema.
Msajili
Kwa upande mwingine alisema inasikitisha
kuona Mahakama inafanya ubaguzi katika usajili wa kesi akiweka bayana kuwa kuna
mbinu zinatumika kwenye usajili.
Bajeti
Kuhusu bajeti na maslahi ya wafanyakazi
wa Mahakama, alisema ataangalia jinsi ya kufanya huku akiitaka Mahakama kuwa
sehemu ya kuchangia pato la Taifa.
Alisema inasikitisha watu wanakwepa kodi
na hata Mahakama inapohukumu utekelezaji au ukaziaji hukumu linakuwa tatizo.
“Serikali imeshinda kesi za kodi tangu
mwaka 2001 zinazofikia Sh trilioni 7.5 zimepakiwa pamoja na hukumu za kwanza
kutolewa na tukashinda, najua mnahitaji mshahara mkubwa na marupurupu, ila isiwe
sababu ya kutetea wakwepa kodi,” alisema.
Alisema kuna utaratibu wa kesi kuwekewa
pingamizi huku kesi kama hizo za kodi katika nchi nyingine, zinasikilizwa na
kutolewa uamuzi haraka bila kuangalia mhusika ni nani.
Alisema wapo majaji ambao kokote wanakopita
wanakubalika kutokana na kazi zao zilizotukuka ila wapo ambao kila kesi
wakipelekewa wanashindwa, hao hawafai na wanapaswa kuchunguzwa.
Alisema inashangaza Mahakama kutoa
hukumu zinazofanana kwa watuhumiwa wa sekta hiyo, na kutolea mfano mahakimu 28
walioshitakiwa kwa rushwa lakini wote wakashinda.
Halikadhalika suala la Escrow ambalo lilihusisha
majaji lakini hakuna hatua iliyochukuliwa, jambo ambalo linajenga imani mbaya
kwa wananchi.
Rais alisema katika mazingira yanayoibua
maswali, mwaka jana majaji 80 waliomba likizo, licha ya Serikali kutotoa fedha
za likizo kwa majaji 74, wapo ambao waliokwenda nje ya nchi na kukaa mwezi
mmoja hivyo kuibua maswali ya nani aliwalipia kwenda nje.
Kaimu Jaji Mkuu
Awali akizungumza katika sherehe hizo,
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alisema mahakama imejipangia
kutekeleza mkakati wa miaka mitano wenye lengo la kubadilisha muhimili huo na
kufanikisha mpango wa Taifa wa miaka mitano
Alisema kuna maeneo matatu ya mpango ambayo
ni utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, upatikanaji haki kwa
wakati na uimarishaji imani ya wananchi na ushirikishwaji wadau kwenye shughuli
za kimahakama.
Alisema moja mikakati yao ni kuona
muhimili huo unakuwa chachu ya kukuza uchumi ikiwa ni kuungana na Benki ya
Dunia ambayo inazitaka mahakama kuwa hivyo.
“Napenda
kuwapongeza wananchi na wadau wote ambao kwa pamoja tumekuwa tukishirikiana
kuhakikisha kuwa changamoto zilizo katika mahakama zinatatuliwa,” alisema.
Mwenyekiti wa TLS, John Seka alisema
wamejipanga kushirikiana na Serikali kuhakikisha dhana ya uchumi wa nchi
inatekelezeka.
Aidha, Seka alimwomba Rais kumthibitisha
Profesa Juma kuwa Jaji Mkuu kwa alichodai kuwa na sifa zote ambazo ni weledi na
uwezo.
0 comments:
Post a Comment