Fidelis Butahe, Dodoma
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye ametangaza kuanza kutumika kwa Sheria ya Huduma za Habari
ya Mwaka 2016 sambamba na kanuni zake zinazobainisha kiwango cha elimu kinachotakiwa
kwa waandishi wa habari ni kuanzia stashahada na kuendelea.
Amesema kanuni hizo zimetoa kipindi cha
mpito cha miaka mitano ya utekelezaji wa mambo mbalimbali, ikiwemo kiwango
hicho cha elimu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
katika ukumbi wa Ofisi za Bunge mjini Dodoma, Nape alisema Sheria hiyo imeanza
kutumika tangu Desemba 31 mwaka jana baada ya Rais John Magufuli kuisaini huku
kanuni zake zikichapishwa katika Gazeti la Serikali (GN) la Februari 3 mwaka
huu,
“Kipindi cha mpito kimeanza Januari
mwaka huu hadi Januari mwaka 2021 kwa waandishi wasiokuwa na sifa za elimu
wakasome. Sheria hii pia inaleta mfumo madhubuti wa kulinda haki za wanahabari
kukusanya, kuhariri na kusambaza habari zao kwa uhuru. Vyombo vya habari sasa
vitatekeleza haki yao hii ya kikatiba bila vikwazo visivyokuwa na sababu,”
alisema Nape.
Alisema umma na wana tasnia
wanakumbushwa sheria hii kwa lengo la kuwa na wanataaluma wanaotekeleza vyema
wajibu wao na kama ilivyo kwa taaluma nyingine, imeweka wajibu kwa wale watakaokiuka
msingi na maadili ya taaluma.
Alisema katika utekelezaji utekelezaji
wa Sheria hiyo kwa taasisi zilizopo, zitaongezewa majukumu au kazi zake
kuhuishwa sambamba na kuanzishwa kwa vyombo vipya.
“Jukwaa la Wahariri (TEF) walitoa maoni
mazuri sana kuhusu suala la elimu. Tumechambua maoni yao na mengine. Wapo
waliotaka iwe cheti, wengine shashahada, baadhi shahada na wapo waliotaka iwe
shahada ya uzamivu. Pia wapo waliotaka iwe mtu yeyote anayejua tu kusoma na
kuandika,” alisema Nape.
“Serikali imesimama katikati ya maoni
yao. Sifa ya chini kabisa kwa kuanzia itakuwa ni stashahada ya uandishi wa
habari. Hata hivyo Serikali imetoa kipindi cha mpito cha miaka mitano kwa
wanahabari waliopo sasa na wanaotaka kuingia katika taaluma hii, ili wawe na
sifa stahiki.”
Kuhusu kiwango cha elimu kwa wahariri wa
habari alisema, “Nalo lilikuwa na mjadala mpana sana, lakini niwapongeze sana
TEF waliwasilisha mapendekezo mazuri na sisi tukaona tuliache kwa wamiliki wa
vyombo husika. Wao ndio wataamua.”
Alisema kanuni za sheria hiyo zinaeleza
utekelezaji wake ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuanzisha gazeti na masuala
mengine huku akisisitiza kuwa vitambulisho vya waandishi wa habari
vinavyotolewa kila mwaka na Idara ya Habari Maelezo vitaendelea kutolewa bila
kuzingatia kiwango cha elimu hadi hapo kipindi cha mpito kitakapomalizika.
0 comments:
Post a Comment