Salha Mohamed na Abraham Ntambara
CHAMA cha ACT Wazalendo kimemtaka Rais
John Magufuli kutumia mamlaka yake kikatiba kutangaza janga la ukame na hali
mbaya ya chakula nchini.
Aidha kimeitaka Serikali kuchukua hatua
madhubuti dhidi ya baa la njaa.
Hatua ya chama hicho inafuatia kile
ilichoeleza kutoridhishwa na hatua ya Serikali katika kuzuia baa la njaa, huku
ikikikusanya takwimu ya bei za vyakula nchini.
Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii wa
chama hicho, Janeth Rithe alieleza hayo jana Dar es Salaam.
Alisema hali ya chakula nchini bado haijatengamaa
na kwamba ACT hakiridhishwi na hatua ambazo Serikali imechukua katika kuzuia
tishio hilo la baa la njaa.
“Tumeshtushwa na taarifa mpya za
Serikali juu ya hali ya chakula nchini, hasa juu ya uhaba wa vyakula, tishio la
baa la njaa na mfumuko mkubwa wa bei za vyakula, na hali ya ukuaji wa kiuchumi
wa wananchi kwa ujumla,”alisema.
Alisema Sekretarieti ya ACT ilikusanya
takwimu kwa wiki mbili kuhusu bei ya vyakula mbalimbali nchini na kubaini bei
ya unga, maharage na vyakula vingine imepanda kwa takriban Sh1,100 kutoka Sh 900
kwa kilo kwa miezi mitatu iliyopita hadi Sh 2000 mwezi huu.
Rithe alisema uamuzi wa Serikali ya Chama
cha Mapinduzi(CCM) kwa kupunguza bajeti ya ruzuku ya mbolea kutoka Sh. bilioni
78 mwaka 2015/16 hadi Sh. bilioni 10 mwaka 2016/17 haukuwa sahihi na kwamba
sasa inapaswa kuchochea tija kwenye kilimo.
“Uamuzi huo umechangia kuwapunguzia
wananchi uwezo wa kuzalisha.Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa
nchi zinazotumia mbolea kwa kiwango kidogo zaidi ulimwenguni.
“Ni kwa sababu hii takwimu za Serikali
zilizotolewa na Waziri wa Fedha zinaonesha kuwa kwa mwaka 2016 kasi ya ukuaji
wa kilimo imeshuka kutoka asilimia 2.5 hadi 0.6,”alisema.
Alisema Serikali inapaswa kutenga fedha
kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa kilimo cha mvua zisizotabilika.
Kwa mujibu wa ACT, Serikali inatakiwa
kujenga maghala ya kutosha pamoja na Bunge kuongeza bajeti ya hifadhi ya
Chakula ya Taifa.
Kuhusu Benki Kuu, ACT ilisema taarifa za
benki hiyo kuhusu hali ya uchumi wa nchi kwa Desemba 2016 zinaonesha kuna
mfumuko mkubwa wa bei za vyakula, hasa chakula kikuu kwa Watanzania.
Alitaja baadhi ya vyakula kama mahindi,
ambapo mfumuko wa bei yake umekua kwa zaidi ya asilimia 30 na kusababisha
kupanda kwa gharama za maisha za wananchi wote.
0 comments:
Post a Comment