*Ni Vanessa Mdee, Tunda Sabasita, wakacha
*Makonda atoa agizo kukutana nao
Jumatatu
Salha Mohamed
WASANII wawili Vanessa Mdee na Tunda
Sabasita ‘Video Queen’ ni miongoni mwa watuhumiwa wapya walioongezwa kwenye
orodha ya walioitwa Polisi kwa mahojiano, kutokana na kutajwatajwa kwa utumiaji
na uuzaji wa dawa za kulevya.
Mbali na wasanii hao wawili, wanne kati
ya watano wa mwanzo kuitwa, walifika jana kwenye Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es
Salaam kwa mahojiano, wakiongozwa na aliyekuwa Mnyange wa Tanzania 2006, Wema
Sepetu, ambaye alionekana akilia kituoni hapo muda mwingi.
Wasanii wengine waliowasili kituoni hapo
kwa mahojiano ni Khalid Mohamed ‘TID’, Hamidu Chambuso ‘Nyandu Tozi’ na mwingine
aliyetajwa kwa jina la Babuu wa Kitaa.
Akizungumza jana Dar es Salaam baada ya
kuwasili kwa wasanii hao Polisi, Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda alitaja orodha ya
watuhumiwa watano iliyoongezeka, akiwemo Vanessa na Tunda. Wengine ni maaskari
Mudy Zungu, Fadhil na Beni.
”Hawa watatu Kamishna waunganishe kwenye
orodha ya wengine muanze kushughulika nao, kuna mwingine anahangaika kununua
nyumba Kigamboni kupitia hizi fedha za dawa za kulevya, mimi nipo na
nitaendelea kuwepo na tutafanikiwa,” alisema.
Makonda alimtaka Kamanda wa Polisi wa Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro ifikapo Jumatatu awe amekamata watuhumiwa
waliotakiwa kufika kituoni hapo jana lakini hawakufika.
“Vita hivi haviishi leo, vitakwisha dawa
zitakapokwisha lakini vita hivi si vya Kamishna Sirro, si vya Rais Magufuli
(John), wala Makonda bali ni kila mkazi wa Dar es Salaam, kwani tunaishi nao,
tunakula nao, tunacheza nao na wengine ni wafadhili wetu.
“Nimegundua na limenishitua na
litafanyiwa kazi, huwezi kuwa na askari aliyekwenda kukamata dawa za kulevya,
halafu akachukua na kuuza, sasa alimwuzia nani?
“Halafu huyo huyo askari bado yumo kwenye
utumishi, anahudumia wananchi kama askari ni sawa na majambazi tu,” alisema.
Alisema hawawezi kuendelea kuwa na
baadhi ya watumishi wanaochafua Jeshi la Polisi na kuchafua heshima ya Kamanda
Sirro.
“Askari wengine ndani ya hizi wiki mbili
walichukua fedha za dawa za kulevya Sh bilioni moja na kugawana, na wanaishi
kwa raha mjini wakati sisi na Rais Magufuli tunapambana na dawa ili ziishe,
askari wanafanya hiyo kazi. Mimi mtandao huu lazima utokomee.
“Wananchi wanazidi kuhamasika na kuona
kumbe Serikali ya Magufuli inatokomeza dawa, kwa imani zao wanaendelea kutoa
taarifa, nina majina ya watu watano na wa sita yuko China anaingiza dawa mwezi
huu, nimeagiza Uhamiaji akiingia tu wamtie nguvuni,” alisema Makonda.
Aliwataka wananchi watambue kuwa vyombo
vya Dola viko imara na hawatasita kuwachukulia hatua wanaokwenda kinyume na
maadili ya utumishi.
Alisema wananchi wana wajibu wa
kuhakikisha wanashiriki mapambano hayo na kushinda.
Alisema jambo hilo si la wasanii peke
yao bali wengine wa kawaida na kumtaja Omary Sanga kusababisha zaidi ya
asilimia 65 hadi 75 ya Watanzania kufungwa China.
“Sasa hivi yuko Dubai anajiandaa kwenda
China, lakini mkono wa Magufuli ni mrefu tutamkamata, wengine Kashozi, Amani,
Halidali Kavila, Tunda hawa wote nawahitaji Jumatatu saa mbili asubuhi akiwamo
dada yangu kipenzi Vanessa,” alisema.
Makonda alisema furaha yake ni kuona
mkoa unapona ili hata mikoani kuwe salama na heshima ya mkoa iliyoasisiwa na
hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume inarudi.
Kamanda Sirro alisema tayari Jeshi lake limeunda
timu maalumu ya kushughulika na wanaojihusisha na dawa za kulevya chini ya
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Mkoa huo, Makonda.
“Timu hii imeundwa na idara zote si polisi
peke yao, lengo ni kutokomeza dawa za kulevya Dar es Salaam, tuko vizuri,” alisema.
Sirro alisema katika tano walikamata
kete tatu huku akibainisha kuwa operesheni hiyo ni endelevu.
Alisema hadi sasa polisi 10 wamekamatwa huku
wawili wakiwa nje ya mkoa na taratibu za sheria zinafuatwa ili wakamatwe.
Idadi hiyo inafanya jumla ya askari kuwa
15 wakidaiwa kujihusisha na uuzaji na utumiaji dawa za kulevya.
Wema alifika kituoni hapo mapema jambo
lililofanya waandishi kutomwona wakadai amepita mlango wa nyuma.
Kutokana na hali hiyo, iliwalazimu polisi
kumtoa nje na kupanda gari namba T 811 DJK na kuzunguka jengo hilo na kuingia tena
na waandishi kumwona na kumpiga picha naye akashindwa kuhimili na kulia.
Wasanii wengine waliowasili kituoni hapo
ni TID, Nyandu tozi na Babuu wa Kitaa.
0 comments:
Post a Comment