Iddi Azan |
ALIYEKUWA Mbunge wa Ilala, Iddi Azan na
Mmiliki wa Sea Cliff Casino, wamekwenda kuripoti kwenye Kituo Kikuu cha Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda.
Juzi Mshauri Mkuu wa Kampuni ya
Quality Group, Yusuph Manji na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat
Gawajima walikuwa wa kwanza kuripoti kituoni hapo kama walivyoahidi.
Makonda alitaka watu 65 wakiwamo hao
kuripoti kituoni hapo na kukutana na Kamati ya Upelelezi iliyoundwa na Mkuu wa
Mkoa huo, ili wahojiwe kuona kama wanahusika na dawa za kulevya au la.
Licha ya Manji na Gwajima kuripoti juzi,
jana saa 3:06 gazeti hili lilishuhudia Azan akiwasili akiwa na gari aina ya
Jeep kuhojiwa akifuatana na baadhi ya watu wake wa karibu.
Aidha, saa 10:25 mmiliki wa Sea Cliff
Casino aliwasili kituoni hapo akiwa na gari namba T 356 DHU aina ya Noah na
baadhi ya watu ambao walimbebea kiti cha kukalia kwa kuwa ni mzee.
Akizungumzia waliofika juzi na jana kwenye
kituo hicho ambao ni wanane, Kamishna wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema operesheni hiyo inaendelea vizuri na
kushukuru wana Dar es Salaam ambao
wanaendelea kutoa taarifa kuhusu masuala hayo ili kuondokaa na uhalifu wa aina
hiyo.
“Hadi jana kati ya watu 65 waliotakiwa
kuripoti kituoni hapo kwa ajili ya kuhojiwa, ni wanne akiwamo Mchungaji wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima Josephat Gwajina na Mshauri Mkuu wa Kampuni za
Quality Group, Yusuph Manji ambao jana (juzi) waliripoti na upelelezi
uliendelea hadi usiku.
“Wamelala mahabusu na unaendelea
kufanyika, kimsingi agizo ninalotoa kama Makonda alivyosema, wahusika wajitokeze
kwa kuwa ofisi ya upelelezi iko wazi,” alisema.
Kamishana Sirro alisema kwa sasa hawezi
kuweka wazi majina ya waliohojiwa na kueleza kuwa waliotajwa wanapaswa kuacha
uoga wajitokeze.
Alisema wanaojihusisha na vitendo hivyo
wataendelea kubaki mahabusu na watakaoonekana hawahusiki, wataachwa na kusisitiza kwa ambao hawajafika wafike.
“Huna sababu ya kuwa na uoga maana watu
wanapiga simu sana mmefanya nini na wengine wanatuma ndugu zao, hivyo huna
sababu ya kumtuma ndugu yako kuja kumwona Sirro, suala la msingi umetajwa na
unajua ni msafi huna makandokando, ripoti kwenye Kamati itakuhoji na kupeleleza
mambo yote ikiona huhusiki itakuacha,” alisema.
Alisema kimsingi hadi sasa baadhi ya
watu wameripoti na ataelezea zaidi kesho (leo) na kwamba wengine wanaendelea kufika
kituoni hapo kuonana na timu ya upelelezi.
Katika hatua nyingine, alisema kwenye mwendelezo
wa operesheni dhidi ya wauzaji na watumiaji
wa dawa za kulevya, Jeshi hilo limekamata watuhumiwa 11 wakiwa na kete 38 za
bangi na magunia sita ya bangi.
0 comments:
Post a Comment