*Awashitaki pia Kamanda Sirro na Mpelelezi Mkuu Wambura
*Awakilishwa na Kurugenzi ya Haki za Binadamu ya
Chadema
Waandishi Wetu
Freeman Mbowe |
KIONGOZI wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amekwenda
mahakamani kufungua kesi ya kikatiba dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda.
Taarifa
iliyopatikana jana ilisema Mbowe alifungua kesi hiyo dhidi ya Makonda, Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Camilius Wambura
na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro.
Kesi hiyo
ilisajiliwa kama kesi ya kikatiba namba moja ya mwaka 2017 kwenye Mahakama Kuu
ya Tanzania Masjala ya Katiba (Masjala Kuu).
Katika kesi
hiyo kwa mujibu wa chanzo cha habari, Mbowe anaiomba Mahakama Kuu itamke kuwa
Mkuu wa Mkoa hana mamlaka ya kudhalilisha na kukamata.
“Mbowe pia
ameiomba mahakama itengue vifungu vya 5 na 7 vya Sheria ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa kwa kuwa ni batili na vinakiuka haki za Katiba,” kilisema
chanzo cha habari hii.
Katika kesi
hiyo, ilielezwa kuwa Mbowe anawakilishwa na mawakili kutoka Kurugenzi ya
Katiba, Sheria na Haki za Binadamu ya Chadema.
Tuhuma
Juzi Makonda
alimtaja Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, kuwa mmoja wa watu 65 wanaotuhumiwa
kujishughulisha na dawa za kulevya, akimtaka kuonana naye jana kwenye Kituo
Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa mahojiano.
Akizungumza
jana mjini hapa na waandishi wa habari kabla ya kufungua kesi hiyo, Mbowe
alisema hatakwenda kuonana na Makonda na badala yake atamburuta mahakamani kwa
kumchafua.
Alisema
atakwenda Polisi pale tu atakapopewa mwito maalumu wa kisheria unaomtaka kufika
kituoni hapo kutokana na tuhuma hizo.
Mbowe, aliuita
mwito huo wa Makonda kwake kuwa ni wa kijinai hivyo hawezi kuutii mpaka utakapokuwa
wa kisheria.
“Nina mambo
matatu ya kuzungumza; kwanza, nakanusha kwa nguvu zote kujihusisha na biashara
ya dawa za kulevya, kwa sababu katika maisha yangu, sijawahi kujihusisha na
biashara hiyo au hata kutumia dawa za kulevya,” alisema Mbowe.
“Pili, sisi
wapinzani, tunakubaliana na mapambano dhidi ya dawa hizo kwa sababu ni hatari kwa
maisha yetu na tunaona vita hivi vilitakiwa vipiganwe miaka mingi iliyopita,
lakini kutokana na sababu mbalimbali, havikupiganwa,” alisema.
Jambo la
tatu kwa mujibu wa Mbowe ni kwamba Makonda si polisi na kwa mujibu wa
sheria hana mamlaka ya kuita mtu Polisi ingawa ni kiongozi wa mkoa.
Alisema yeye
ni Mbunge na kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani, ni baba mwenye mke na watoto,
hivyo hawezi kukubali ‘mjinga’ mmoja amchafue bila sababu.
“Who is (ni
nani) Makonda? … siwezi kwenda Polisi kuhojiwa hadi watakaponiita kwa kufuata
utaratibu wa kisheria. Kwa hiyo, nitamfungulia mashitaka ya kunikashifu wiki
ijayo yeye kama yeye na si kama Jamhuri
kwa sababu sina tatizo na Jamhuri,” alisema.
“Katika
hili, nitadai haki yangu katika mahakama za ndani na ikibidi za nje. Makonda
hana fedha za kunilipa kutokana na alivyonichafulia jina,” alisema Mbowe.
Alisema
atamfungulia mashitaka si kwa sababu ana shida na fedha, bali kutokana na
kuchafuliwa jina.
Huku
akifuatana na wabunge takribani 30 wa Upinzani, Mbowe alisema: “Nimejenga sifa
yangu kwa miaka mingi na nitaendelea kuilinda kwa nguvu zote. Mimi si mtoto
mdogo na hili ndilo tatizo la kuwapa watu vyeo wasio na busara.
“Kamwe
huwezi kupambana na dawa za kulevya kwa kutaka sifa, nitamshitaki kwa sababu
yeye ndiye ana kiherehere,” alisema.
Alisema
hakuna anayemwogopa Makonda, kwa sababu tu yuko karibu na Rais John Magufuli na
kusisitiza kuwa hana fedha ya kumlipa.
Akizungumzia
utaratibu unaotumiwa na Makonda kutaja wahusika wa dawa za kulevya, alisema
haufai kwa sababu unawafanya waanze kuchukua hadhari.
Alisema ana
wasiwasi na wanaotajwa kwa maelezo kuwa baadhi yao wakiwamo walioelezwa kuwa
wamiliki wa Yatch Club na Sleep Way, “hayo maeneo si ya mtu mmoja, yanamilikiwa
kwa ubia na watu wengi.”
Akizungumza kwenye
mkutano huo, kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto
Kabwe alisema kama Mbowe angekuwa anajihusisha na dawa za kulevya, yeye
angekuwa mshirika wake, kwa sababu amefahamiana naye tangu akiwa mdogo.
Alimpongeza
kwa kugoma kwenda kuhojiwa Polisi. “Ningemshangaa kama angekwenda, maana
Makonda hana mamlaka hayo. Makonda aseme ni sheria ipi inampa mamlaka ya kutangaza
watu na kuwataka wakaripoti Polisi.”
Alibainisha
kuwa anaposhambuliwa Mbowe ni sawa na kushambuliwa wapinzani wote na kubainisha
jinsi alivyoibuliwa kwenye siasa na Mwenyekiti huyo wa Chadema.
Mwanzoni mwa
wiki, Makonda aliitisha mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam na kutaja watu 65 aliodai
wanajihusisha na dawa za kulevya.
Pamoja na
Mbowe, wengine ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, Mbunge
wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan na mfanyabiashara Yusuf Manji.
Sirro
Baada ya
kauli ya msimamo wa Mbowe, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Sirro jana alitangaza kwamba Jeshi hilo litamtia nguvuni
Mbowe asipotii agizo la kwenda kituoni hapo kuhojiwa.
Kamanda Sirro alisema hayo wakati
akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari, uamuzi wa Mbowe kukataa kuripoti
kituoni hapo kama alivyotakiwa na Makonda.
Kwa mujibu wa Kamishna Sirro, Jeshi hilo
litahakikisha linamfuata kokote aliko, kwa kukaidi mwito wa kuhojiwa, ili
kupata ukweli kuhusu kutajwa kuhusika na dawa hizo.
Alisema kwa kawaida mwenye hekima na busara
hutii amri kwa kuitika mwito akiitwa, lakini akikaidi lazima achukuliwe hatua,
hivyo kama Mbowe amekaidi alisema sheria itachukua mkondo wake.
“Kama ikitokea mawakili na wanasheria
wake wakaleta taarifa zenye sababu za msingi za kutoripoti tutamwacha na
kumhoji hata kesho (leo) kwani lengo letu ni kumhoji ili kujua ukweli, lakini
kama ameamua kukaidi msimamo wetu uko palepele,” alisema Kamanda Sirro.
*Imeandikwa
na Fidelis Butahe, Dodoma na Celina
Mathew, Dar
0 comments:
Post a Comment