Fidelis Butahe, Dodoma
AMRI za baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya nchini
kutaka Jeshi la Polisi kukamata watendaji wa Serikali, wanahabari na watu wa
kada mbalimbali na kuwasweka rumande kwa madai ya kufanya makosa, zimepingwa na
wabunge.
Wabunghe hao walifikia hatua hiyo jana kwa maelezo
kuwa ni ukiukwaji wa sheria za utumishi wa umma na utawala bora.
Bila kujali itikadi zao, wabunge hao walisema
utawala bora ni nguzo muhimu katika ujenzi wa jamii yenye umoja, usawa,
mshikamano, audilifu na uwajibikaji na kuwataka wateule hao wa Rais kuacha
kujigeuza miungu watu.
Wabunge walitoa kauli hiyo kwenye mjadala wa
taarifa ya Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, ambayo ilitoa
mifano ya amri za wakuu hao wa mikoa na wilaya licha ya kutowajata majina, huku
ikisisitiza kuwa wanachokifanya si sahihi.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo ya mwaka
2016/17, mjumbe wa Kamati hiyo Esther Mahawe alisema siku za hivi karibuni
watendaji wa Serikali wamechukua nafasi ya mhimili wa Mahakama kwa kuhukumu na
kuwatia hatiani baadhi ya watumishi wa umma.
“Wanafanya hivyo bila kujua, kwamba wanakiuka
msingi wa Katiba waliyoapa kuilinda. Ibara ya 13 (6) na (2) ya Katiba inazuia
mtu anayeshitakiwa kwa kosa la jinai, kutendwa kama mwenye kosa hilo hadi
itakapothibitishwa na Mahakama yenye mamlaka,” alisema.
“Kwa hiyo, hatua ya Mkurugenzi wa Halmashauri kumwamuru
mwalimu wa sekondari adeki darasa mbele ya wanafunzi wake, au Mkuu wa Mkoa
kutumia lugha zisizofaa kwa watendaji ni kuwadhalilisha na kuvunja misingi ya
Katiba,” aliongeza.
Mahawe alisema wateule hao wamekuwa wakitumia
vibaya mamlaka waliyopewa kuamrisha watumishi wa umma kuwekwa ndani kwa makosa yasiyostahili
adhabu hiyo.
“Ipo mifano kadhaa ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa mmojawapo
nchini kuamuru Daktari wa Mkoa awekwe rumande kwa sababu hakutangaza kuwapo
kipindupindu,” alisema.
Alisema Mkuu wa Wilaya moja mkoani Dar es Salaam
aliamuru watumishi waliochelewa kazini wawekwe ndani huku Mkuu wa Wilaya moja
Arusha akiamuru mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni awekwe ndani kwa
kuandika habari kuhusu kero za ukosefu wa maji, ikidaiwa ni uchochezi.
“Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 imeweka
masharti muhimu kwa Mkuu wa Mkoa au Wilaya ikiwa atahitaji kutumia mamlaka ya
kuamuru mtu akamatwe,” alisema.
Alibainisha kuwa vifungu hivyo vinaeleza, kwamba
atafanya hivyo pale tu atakapokuwa amejihakikishia kuwa kosa lililotendwa na
mhusika athari zake huwa ni kukamatwa na kushitakiwa.
“Kamati inatambua juhudi za Serikali kurejesha
nidhamu ya uwajibikaji katika utumishi wa umma…kamwe haiwezi kutetea watumishi
wazembe, hata hivyo watumishi wazembe na wasiotekeleza majukumu yao wachukuliwe
hatua za kinidhamu na kiuwajibikaji kwa mujibu wa taratibu zilizopo,” alisema.
Wachachamaa
Mbunge wa Muheza (CCM), Adadi Rajabu alisema wakuu
hao wa mikoa na wilaya wanatumia madaraka yao vibaya na kubainisha kuwa hilo ni
tatizo la kukosa semina elekezi baada ya kuteuliwa na Rais.
“Wakibishana na mtu kwenye kikao wanaamuru awekwe
ndani, huo si utaratibu kabisa, kwa sababu hata polisi wanapata kozi ya miezi
sita kufundishwa namna ya kukamata watu. Suala hili liangaliwe, litaleta
shida,” alisema.
Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe alisema
wateule hao wa Rais katika baadhi ya maeneo ni kero kutokana na kukosa
ushirikiano wa kutosha kwa viongozi wengine jambo linaloleta mgongano wa
utendaji.
“Wanatakiwa kusoma sheria kabla ya kuchukua hatua
kwa wananchi. Wanatakiwa kujua ni wakati gani wanakuwa na mamlaka ya kutoa amri
ya kukamata mtu,” alisema Richard Mbogo (Nsimbo-CCM).
Kwa upande wake Juma Nkamia (Nchemba -CCM) alisema
wamekuwa wakitoa kauli zisizofaa kwa viongozi wa maeneo yao na kuibua
mgawanyiko.
Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara
alisema wakuu hao wa mikoa na wilaya wamejivika kofia ya utais katika maeneo
yao ya kazi jambo ambalo si sahihi.
“Wanatoa amri za vitisho kwa kweli ingawa mimi
namtambua Rais mmoja tu, John Magufuli,” alisisitiza Waitara.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi,
George Simbachawene alisema, “"Ni kweli wapo baadhi ya wakuu wa mikoa na
wilaya wanakiuka utaratibu wa kazi, lakini tufahamu kuwa wao ni binadamu. Kama
kuna kiongozi anakwenda kinyume na sheria ni suala la mawasiliano tu
arekebishwe.”
Pia, alisisitiza kuwa wana mamlaka kisheria kupewa ulinzi
wa askari saba hadi 11 kwa mujibu wa sheria.
Baadhi ya matukio
Aprili 7 mwaka jana, mkuu wa Wilaya ya Chato,
Shaaban Ntarambe alimuweka mahabusu mwandishi wa gazeti moja la kila siku
wilayani humo kwa madai ya kuingia hospitali ya wilaya bila kibali chake.
Desemba 12 mwaka huu, mwandishi mwingine wa Kituo
kimoja cha Televisheni mkoani Arusha, alikamatwa na kushikiliwa na polisi
katika kituo cha polisi cha Usa River wilayani Arumeru kwa tuhuma za kuandika
habari zinazodaiwa kuwa ni za uchochezi huku agizo hilo likitolewa na mkuu wa
wilaya hiyo, Alexander Mnyeti.
Desemba Mosi mwaka huu, mkuu wa wilaya ya Kibaha,
Assumpter Mshama alimbana mwandishi wa gazeti mola la kila siku akimtaka aombe
radhi kutokana na habari aliyoiandika kuhusu kutofanyika usafi wa mazingira
kila mwisho wa mwezi kwa madai kuwa habari hiyo inalenga kumgombanisha na Rais
Magufuli.
Naye mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
alipokuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni aliwaweka rumande maofisa ardhi wa wilaya
hiyo kwa saa sita kutokana na kuchelewa kufika katika eneo la Sangwe kata ya
Wazo walipokuwa wamekubaliana kukutana kwa ajili ya kutafuta suluhisho la
migogoro ya ardhi katika eneo hilo.
0 comments:
Post a Comment